OKTOBA 15, 2024
BRAZILI
Mahakama Kuu ya Brazili Yaunga Mkono Haki ya Mgonjwa ya Kuchagua Matibabu
Mahakama Yawaunga Mkono Mashahidi wa Yehova Katika Kesi Mbili
Septemba 25, 2024, Mahakama Kuu ya Brazili ilitoa uamuzi muhimu ambao unaunga mkono haki ya wagonjwa walio watu wazima kukataa kutiwa damu mishipani na badala yake kuchagua matibabu yasiyohusisha kutiwa damu mishipani. Mahakama hiyo pia ilitoa uamuzi kwamba Wizara ya Afya inapaswa kuhakikisha kwamba wagonjwa ambao wanakataa kutiwa damu mishipani kwa sababu za kibinafsi au kwa msingi wa imani yao ya kidini, wanaweza kupata matibabu ambayo hayahusishi kutiwa damu mishipani.
Uamuzi huu ulitolewa kwenye kesi zilizowahusisha Mashahidi wawili wa Yehova nchini Brazili. Mwaka wa 2018, madaktari wa Dada Malvina Silva walikataa kumfanyia upasuaji wa moyo uliokuwa umeratibiwa alipokataa kutia sahihi fomu ya kuwaruhusu madaktari hao kumtia damu mishipani. Ilimchukua Malvina miaka miwili hivi kupata matibabu yaliyoheshimu imani yake.
Mwaka wa 2014, Ndugu Heli de Souza alikuwa ameratibiwa kufanyiwa upasuaji. Hata hivyo, hospitali iliyokuwa ikimpa matibabu haikuwa na vifaa vya kutosha vya kufanya upasuaji huo bila kumtia damu mishipani. Isitoshe, Heli alipoomba kuhamishiwa kwenye hospitali nyingine ambayo ilikuwa tayari kumfanyia upasuaji huo kwa njia itakayoheshimu imani yake, Idara ya Afya nchini humo ilikataa ombi lake. Heli bado anasubiri kufanyiwa upasuaji huo. Mashahidi wengi wa Yehova nchini Brazili wanakabili changamoto kama hizo, kutia ndani kutiwa damu mishipani bila hiari yao.
Hakimu Luís Roberto Barroso ambaye ni rais wa Mahakama Kuu ya Brazili, alisema hivi alipokuwa akitoa uamuzi huo: “Haki ya kukataa kutiwa damu mishipani kwa msingi wa imani ya kidini inatokana na kanuni za kikatiba za uhuru wa kidini na heshima kwa binadamu. Hivyo, kuhusiana na haki ya kuishi na kuwa na afya nzuri, [Mashahidi wa Yehova] wana haki ya kupata matibabu mbadala [na] wana haki ya kukataa matibabu yanayohusisha kutiwa damu mishipani kwa msingi wa haki ya kufanya uamuzi wa kibinafsi.”
Uamuzi huu wa karibuni zaidi umeweka kiwango ambacho mahakama zote nchini Brazili zitahitaji kufuata inapohusu kuheshimu haki ya mgonjwa ya kufanya uamuzi wa kibinafsi kuhusu matibabu atakayopata. Uamuzi huo unafanana na uamuzi ambao ulitolewa na Mahakama Kuu katika nchi zingine, kutia ndani Australia, Kanada, Japani, Afrika Kusini, na Marekani. Pia, uamuzi huo unafanana na uamuzi uliotolewa Septemba 17, 2024 na Baraza Kuu la Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu, ambao uliweka kiwango ambacho nchi 46 za Ulaya zinahitaji kufuata. Uamuzi huo unahusu kuheshimu haki ya mgonjwa ya kufanya uamuzi wa kibinafsi kuhusu matibabu atakayopata.
Tunafurahi kwamba Mahakama Kuu ya Brazili ilitoa uamuzi unaoheshimu imani za raia wake na haki yao ya kufanya maamuzi ya matibabu watakayokubali.