Hamia kwenye habari

MEI 23, 2018
ITALIA

Chuo Kikuu cha Padua Kimefanya Kongamano la Kihistoria la Kuzungumzia Maendeleo ya Matibabu Yasiyohusisha Damu

Chuo Kikuu cha Padua Kimefanya Kongamano la Kihistoria la Kuzungumzia Maendeleo ya Matibabu Yasiyohusisha Damu

ROME—Ijumaa, Novemba 24, 2017, wataalamu wa kitiba, wa elimu-maadili ya kibiolojia, na wa kisheria walikusanyika katika Chuo Kikuu cha Padua, chuo kikuu cha pili nchini Italia, kwa ajili ya kongamano lenye kichwa “Watu Wazima Wanapokataa Kutiwa Damu: Kuna Mbinu Zipi Mbadala?—Kuhifadhi Damu Mwaka wa 2017.” Kongamano hilo lilidhaminiwa na mashirika zaidi ya 25 ya kisayansi nchini Italia pamoja na Wizara ya Afya nchini Italia.

Dakt. Luca P. Weltert

Kwa muda fulani, ilionekana kwamba kutia mgonjwa damu mishipani hakuna madhara yoyote na ndiyo mbinu inayoweza kuokoa uhai wakati wa matatizo makubwa ya kiafya au wakati wa upasuaji tata. Lakini wasemaji wengi katika kongamano hilo walipinga wazo hilo. Mmoja wa wataalamu waliozuru, Dakt. Luca P. Weltert, daktari wa upasuaji wa moyo na koo kwenye Hospitali ya Ulaya, Rome, alieleza hivi: “Leo, tumeona kwamba kumtia mgonjwa damu kunaweza kuwa na madhara na katika visa vingi hakuna uhitaji wa kuongeza damu.”

Dakt. Weltert na madaktari wengine walifikia mkataa huo kwa sababu ya muda walioshughulikia visa kama hivyo na vilevile uthibitisho kutokana na uchunguzi wa kisayansi unaoonyesha uhusiano kati ya kumtia mtu damu mishipani na kuongezeka kwa vifo, matatizo ya kiafya, kukaa muda mrefu hospitalini, na madhara mengine makubwa kwa afya ya anayetiwa damu. a

“Leo, tumeona kwamba kumtia mgonjwa damu kunaweza kuwa na madhara na katika visa vingi hakuna uhitaji wa kuongeza damu.”—Dakt. Luca Weltert, daktari wa upasuaji wa moyo, Hospitali ya Ulaya, Rome

Uthibitisho kama huo wa kisayansi, pamoja na gharama kubwa na kumtia mtu damu mishipani, umechochea Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) mwaka wa 2010 uzungumzie uhitaji wa kuwa na mbinu ya kuzuia damu nyingi isivuje (PBM). Kufanya hivyo kumeboresha matokeo kwa afya na kumepunguza sana matumizi ya damu. Shirika hilo lilitoa azimio lililohimiza serikali zote 193 ambazo ni washiriki wa shirika hilo watumie mbinu hizo.

Profesa Stefania Vaglio

Profesa Stefania Vaglio, mkuu wa kitengo cha kutia watu damu katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Sant’Andrea, Rome, alizungumzia kwa muda mrefu mbinu hiyo mpya ya PBM, akisema kwamba zamani, matibabu yalitegemea kushughulikia na kutoa damu, lakini sasa “tumeacha kabisa kukazia kuchangia damu na badala yake tunakazia jinsi ya kushughulikia damu ya mgonjwa mwenyewe.” Kusudi moja la PBM ni “kupunguza kuvuja kwa damu kwa kukazia fikira mgonjwa, . . .  na kufanya yote yanayohitajiwa ili kuhakikisha kwamba damu ya mgonjwa haivuji.” Profesa Vaglio pia alieleza kwamba mbinu za kitiba za kuzuia damu ya mgonjwa isivuje “kihalisi zinaboresha matibabu.”

Dakt. Tommaso Campagnaro, daktari wa upasuaji wa Chuo Kikuu cha Hospitali ya Verona, alithibitisha manufaa ya kutumia mbinu mbalimbali kuepuka kumtia mtu damu mishipani. Baada ya kumaliza kuchunguza rekodi za tangu mwishoni mwa miaka ya 1990 zilizohusisha wagonjwa kufanyiwa upasuaji tata sana wa tumbo, alifikia mkataa huu: “Wagonjwa ambao hawakutiwa damu walikuwa na matatizo machache kwa kulinganishwa na wale waliotiwa damu na wachache zaidi walikufa.”

“Wagonjwa ambao hawakutiwa damu walikuwa na matatizo machache kwa kulinganishwa na wale waliotiwa damu na wachache zaidi walikufa.”—Dakt. Tommaso Campagnaro, daktari wa upasuaji, Hospitali ya Chuo Kikuu cha Verona

Profesa Msaidizi Anna Aprile

Dakt. Campagnaro, pamoja na wasemaji wengine waliwashukuru Mashahidi wa Yehova kwa kuwachochea madaktari watafute mbinu mbadala za matumizi ya damu. Anna Aprile, profesa msaidizi wa masomo ya kitiba katika Chuo Kikuu cha Padua, alisema hivi: “Tunawashukuru Mashahidi wa Yehova ambao wamezusha suala la haki ya kukataa kutiwa damu na kuwachochea watu wote walitafakari na kutafuta njia za kutoongeza damu.”

“Tunawashukuru Mashahidi wa Yehova ambao wamezusha suala la haki ya kukataa kutiwa damu . . .”—Anna Aprile, profesa msaidizi wa masomo ya kitiba katika Chuo Kikuu cha Padua

Wasemaji walikuwa na taaluma mbalimbali za kitiba, kama madaktari wa nusukaputi, wa moyo, wa uzazi, wa damu, wa kushughulikia uvimbe, na wataalamu wa magonjwa ya mifupa. Hata hivyo, walikuwa na ujumbe uleule: wataalamu wa kitiba, wanasheria, na watu wa umma wanapaswa kuwa tayari kutumia mbinu za PBM hasa kwa sababu ya habari inayoongezeka iliyochapishwa na mambo yaliyoonwa kutoka kwa wataalamu katika nyanja hizo.

Waliohudhuria kwenye jumba la Morgagni katika Chuo Kikuu cha Padua wakisikiliza.

Dakt. Weltert anasema hivi: “Kurekebisha mishipa ya damu ya moyo ni mojawapo ya upasuaji mkubwa unaoweza kufanya. . . . Ikiwa [upasuaji huo] unaweza kufanywa bila damu, basi upasuaji wowote unaweza kufanywa.”

Wanahabari Wanaweza Kuwasiliana na:

David A. Semonian, Ofisi ya Habari za Umma, +1-845-524-3000

Italia: Christian Di Blasio, +39-06-872941

a Kwa mfano, uchunguzi uliofanywa hivi karibuni katika eneo la Magharibi ya Australia uliochapishwa katika mojawapo ya majarida makuu kuhusu kutia damu mishipani, Transfusion, ulirejelewa wakati wa kongamano hilo. Walioandika uchunguzi huo wanaeleza matokeo ya kujitahidi katika maeneo mengi sana kwa miaka sita kutumia programu ya kuzuia damu kuvuja. Walichunguza taarifa za wagonjwa 605,046 waliolazwa kwenye hospitali za rufaa za watu wazima. Matumizi ya sehemu za damu yalipungua kwa asilimia  41 wakati wa uchunguzi huo. Wakati huohuo, vifo vilipungua kwa asilimia 28, muda wa kukaa hospitalini ulipungua kwa asilimia 15, magonjwa yanayotokana na kuwa hospitalini yalipungua kwa asilimia 21, na kupungua kwa asilimia 31 kwa mshtuko wa moyo na kiharusi. Kutumiwa kwa mbinu za kuzuia damu isivuje (PBM) kulihusianishwa matokeo bora zaidi kwa mgonjwa, kupungua kwa matumizi ya damu, na kupungua kwa gharama.