Hamia kwenye habari

APRILI 20, 2022
UBELGIJI

Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu Inawaunga Mkono Mashahidi wa Yehova Nchini Ubelgiji Kuhusu Suala la Kodi

Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu Inawaunga Mkono Mashahidi wa Yehova Nchini Ubelgiji Kuhusu Suala la Kodi

Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu (ECHR) ilifanya uamuzi ambao haukupingwa kwamba serikali ya Ubelgiji iliwatendea Mashahidi wa Yehova isivyo haki kwa kuamua kutoza kodi makutaniko tisa katika Eneo la Mji Mkuu wa Brussels. Uamuzi huo katika kesi ya Christian Assembly of Jehovah’s Witnesses and Others v. Belgium, uliotolewa Aprili 5, 2022, unaweza kulinda uhuru wetu wa kidini si tu nchini Ubelgiji bali pia katika nchi nyingine za Ulaya.

Kufikia mwaka wa 2018, dini zote katika Eneo la Mji Mkuu wa Brussels hazikuwa zikitozwa kodi kwa ajili ya majengo yao ya ibada. Katika mwaka huo, eneo hilo lilibadili sheria zake kuhusu kodi na kuamua kwamba ni dini sita tu “zinazotambuliwa” ambazo hazingetozwa kodi. Sheria hiyo mpya ilimaanisha kwamba Majumba ya Ufalme jijini Brussels yalipaswa kulipiwa kodi kubwa sana ya jumla ya karibu euro 45,000 (dola 49,025 za Marekani) kila mwaka.

ECHR iliamua kwamba kwa kutoa msamaha kwa dini sita tu “zinazotambuliwa” na Serikali, Eneo la Mji Mkuu wa Brussels liliwabagua Mashahidi wa Yehova na kwenda kinyume na Mkataba wa Ulaya wa Haki za Kibinadamu.

Kupitia uamuzi huo, ECHR ilipinga pia dai la serikali ya Ubelgiji kwamba Mashahidi wa Yehova wanapaswa kutuma ombi la kutambuliwa na Serikali. ECHR ilisema kwamba nchini Ubelgiji, Waziri wa Haki ndiye tu aliye na mamlaka ya kuanzisha mchakato wa kuilazimisha dini itambuliwe na Serikali. Na uamuzi wa kukubali au kukataa kuitambua haupaswi kufanywa ovyoovyo na serikali.

Katika uamuzi wake rasmi, ECHR ilisema kwamba mchakato wa kupata utambulisho wa Serikali nchini Ubelgiji “hauna msingi.” Iliongezea kwamba “haipatani na akili kutazamia vikundi vya dini kuwasilisha maombi bila kuhakikishiwa kwamba vitatendewa kwa haki . . . inapohusu kupata msamaha wa kodi.” Mahakama hiyo iliiambia serikali ya Ubelgiji itende “bila ubaguzi” inaposhughulika na vikundi vya kidini kama vile Mashahidi wa Yehova.

Uamuzi wa ECHR unakazia kwamba Serikali haziwezi kuamua ikiwa imani fulani za kidini ni sahihi na jinsi watu walio na imani hizo wanavyopaswa kuabudu. Pia, uamuzi huo utasaidia kuzuia nchi nyingine za Ulaya zisiweke sheria za kodi ambazo zitabagua tengenezo letu.

Tunamshukuru Yehova kwa ushindi wote wa kisheria unaotusaidia kutimiza tamaa yetu ya kulitukuza jina lake.​—Ufunuo 15:4.