Hamia kwenye habari

JE, NI KAZI YA UBUNI?

Uwezo wa Pomboo wa Kutambua Mawimbi ya Sauti

Uwezo wa Pomboo wa Kutambua Mawimbi ya Sauti

 Pomboo wanatoa sauti mbalimbali kisha wanasikiliza mwangwi ili kuamua upande watakaoelekea na kutalii mazingira yao. Wakichochewa na uwezo wa pomboo anayeitwa bottlenose (Tursiops truncatus) wa kutambua mawimbi ya sauti, wanatokeza mifumo itakayotumiwa chini ya maji ili kutatua matatizo ambayo hayawezi kutatuliwa na teknolojia ya sasa.

 Zingatia: Uwezo huo unamwezesha pomboo kupata samaki waliojificha kwenye sakafu ya bahari na pia kutofautisha kati ya samaki na jiwe. Kulingana na Keith Brown, profesa msaidizi katika Chuo Kikuu cha Heriot-Watt, Edinburgh, Scotland, pomboo huyo pia akiwa umbali wa “mita kumi anaweza kutofautisha kati ya chombo kilicho na maji baridi, maji ya chumvi, umajimaji wa sukari, na mafuta.” Wanasayansi wangependa kutokeza vifaa vyenye uwezo kama huo.

Wakiwa umbali wa mita kumi, pomboo wanaweza kutofautisha kilicho ndani ya vyombo

 Watafiti walichunguza sauti wanazotoa pomboo hao na uwezo wao wa kusikia kisha wakajaribu kutokeza kifaa kama hicho. Kilikuwa kifaa kilichojaa mifumo ya kielektroni ya hali ya juu kilichoingizwa ndani ya chombo chenye urefu usiozidi mita moja. Kifaa hicho, kilichounganishwa kwenye chombo kinachoweza kujiendesha chenyewe kinachofanana na kombora aina ya torpedo, kilikusudiwa kuchunguza sakafu ya bahari, kutafuta vitu vilivyozikwa chini ya bahari kama vile nyaya au mabomba ya mafuta, na kuyachunguza bila kuyagusa. Wabuni wake wanaona kitatumiwa kutafuta mafuta na gesi. Kifaa hicho kilichobuniwa kwa kuiga uwezo wa pomboo kitaboresha uwezo wa kukusanya habari wa vifaa vinavyotumiwa sasa chini ya maji, kitawasaidia mafundi kuweka vifaa vya majini mahali bora kabisa, kuchunguza ikiwa vimeharibiwa​—kwa mfano ikiwa kuna nyufa ndogo sana kwenye vyuma vinavyotegemeza mashine za kuchimba mafuta​—au hata kugundua sehemu za bomba zilizoziba.

 Una maoni gani? Je, uwezo wa pomboo wa kutumia sauti ulijitokeza wenyewe? Au ulibuniwa?