Sauti ya “Jiji la Milele”
Sauti ya “Jiji la Milele”
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI ITALIA
Mandhari na sauti ya chemchemi nyingi za Rome, zilimchochea mtungaji Ottorino Respighi kutunga wimbo wenye kichwa “Chemchemi za Rome.” Acheni tutembelee moja kati ya chemchemi hizo za ajabu, inayoitwa Chemchemi ya Trevi.
Tunapotembea kupitia barabara nyembamba inayoelekea kwenye chemchemi hiyo, kisha tunapiga kona, tunaona mandhari yenye kustaajabisha. Chemchemi kubwa inayoitwa Trevi yenye upana wa mita 20 na kimo cha mita 26 imesimama waziwazi katika ua mdogo. Inastaajabisha kama nini kwa chemchemi hiyo kusimamishwa katika sehemu nyembamba kama hiyo!
Ujenzi wa Chemchemi ya Trevi uliidhinishwa na Papa Clement wa 12 na kubuniwa na mchora-ramani Mwitaliano Niccolò Salvi. Ujenzi ulianza mnamo 1732 na kukamilishwa mnamo 1762. Maji ya chemchemi hiyo hutoka katika mfereji wa karne ya kwanza K.W.K. unaoitwa Aqua Virgo, ambao chanzo chake kiko kilomita 13 hivi kutoka jijini.
Chemchemi hiyo ambayo imejengwa kando ya kasri, imebuniwa ili ionekane kama bahari. Sanamu ya Oceanus (au, wengine humwita Neptune) anayetajwa katika hadithi husimama kwa fahari akiwa katika gari lake la kukokotwa na farasi, huku akielekeza maji yanayotiririka chini yake. Maji yanapomwagika kupitia sanamu nyingine na kumwagika juu ya mawe yaliyo chini, yanasikika kama mawimbi yanayopiga fuo. Ua huo una beseni kubwa sana ambalo hufanya ua wote uonekane kana kwamba ni sehemu ya chemchemi hiyo.
Kila siku mamia ya watalii hutembelea ua huo mdogo na kutupa sarafu ndani ya chemchemi hiyo ambayo ni moja kati ya sehemu zinazopendwa sana na watalii huko Rome. Mara moja kwa juma, maji yote huondolewa. Pesa zinazoachwa na watalii, ambazo kwa wastani huwa dola 11,000 kwa juma, hukusanywa na kutolewa kama mchango kwa shirika fulani la kidini la kutoa msaada.
Kama Respighi alivyoamini, ikiwa chemchemi hutoa sauti ya jiji, basi Chemchemi ya Trevi inatokeza sauti kubwa zaidi—ya pekee kati ya chemchemi nyingi zinazopendwa na watu wanaotembelea Rome, linalojulikana kama Jiji la Milele.