Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Matunda Matamu ya Bure Kutoka Msituni

Matunda Matamu ya Bure Kutoka Msituni

Matunda Matamu ya Bure Kutoka Msituni

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI FINLAND

FAMILIA nyingi katika nchi za Skandinavia huko Ulaya, hufurahia kwenda msituni kuchuma beri za mwituni. Kwa mfano, huko Finland watu wanaopenda kutembea msituni wanaruhusiwa kuingia katika eneo lolote lenye msitu, hata ikiwa eneo hilo ni mali ya mtu binafsi, mradi tu wasiharibu chochote au kukaribia nyumba yoyote. Hakuna sheria yoyote iliyoandikwa kuhusu jambo hilo lakini hiyo ni desturi ya Waskandinavia ambayo imekuwapo tangu zamani. Desturi hiyo inamruhusu mtu kuchuma maua ya msituni, uyoga, na beri mahali popote.

Kuna aina 50 hivi za beri za msituni nchini Finland, nyingi kati ya hizo zinaweza kuliwa. Aina tatu za beri zinazopatikana kwa wingi ni bilberry, cloudberry, na lingonberry. *—Ona masanduku katika makala hii.

Beri za rangi na ladha mbalimbali hufanya chakula kipendeze na kiwe chenye lishe. “Beri zinazopatikana katika nchi za Skandinavia hasa wakati wa majira ya kiangazi zina rangi, harufu, madini, na vitamini nyingi,” kinasema kitabu Luonnonmarjaopas (Mwongozo wa Kuchuma Beri za Msituni). Isitoshe, beri zina nyuzinyuzi ambazo zinaweza kusaidia kudhibiti kiwango cha sukari mwilini na kupunguza kiwango cha mafuta mwilini. Pia beri zina kemikali fulani ambazo huzuia kuharibika kwa chembe mwilini na inasemekana kwamba kemikali hizo zinatokeza afya nzuri.

Je, kuna faida ya kuchuma beri msituni? “Kujichumia beri husaidia kupunguza gharama kwani beri huuzwa kwa bei ghali sana dukani. Unapojichumia beri unajua zimechumwa wakati gani,” anasema Jukka, ambaye hufurahia sana kuzichuma. Niina, mke wake anataja faida nyingine, “Tunapoenda kuchuma beri, tunapata nafasi nzuri ya kufurahia mlo pamoja kama familia msituni.”

“Lakini ukiwa na watoto, ni muhimu kuwa mwangalifu ili wasile beri mbaya na kuwa macho ili wasipotee,” Niina anaongezea. Unapaswa kuwa mwangalifu kwani beri fulani zina sumu.

Kama watu wengi wa nchi za Skandinavia, Jukka na Niina hufurahia mazingira ya msituni. “Ninapenda sana misitu,” anasema Niina. “Huko kuna utulivu wenye kuvutia na hewa safi ambayo huburudisha akili yangu. Nao watoto pia hufurahia sana kuwa huko.” Jukka na Niina wamegundua kwamba utulivu wa msituni unawaruhusu kutafakari na kuzungumza wakiwa familia.

Beri huwa na lishe na ladha nzuri zinapoliwa mara tu baada ya kuchumwa. Lakini beri huoza haraka. Ili watu wafurahie beri wakati wa majira ya baridi kali, lazima zihifadhiwe. Zamani, watu walihifadhi beri katika maghala ya chini ya ardhi, lakini siku hizi zinahifadhiwa katika friji zenye barafu. Beri nyingi hutumiwa kutengeneza jemu na maji ya matunda.

“Inapendeza kama nini, wakati wa majira ya baridi kali sana, kuchukua chupa yenye beri zilizohifadhiwa na kujikumbusha majira ya kiangazi yaliyopita na kukufanya utazamie majira ya kiangazi yatakayofuata,” anasema mwandishi kutoka Sweden katika kitabu Svenska Bärboken (Kitabu cha Beri za Sweden). Beri hutumiwa katika njia mbalimbali. Wakati wa kiamsha kinywa, zinaweza kuliwa na maziwa ya mtindi, granola, au uji. Beri za msituni zinazoburudisha hutumiwa kutengeneza vyakula vitamu vinavyoliwa baada ya mlo. Hizo pia hutumiwa kutengeneza rojo ya beri au jeli ambayo huliwa na milo mingi.

Watu wengi hununua beri madukani. Lakini hebu wazia ukiwa msituni siku isiyo na mawingu, ukivuta hewa safi, na kufurahia amani na utulivu huku ukitafuta beri tamu zenye rangi nzuri. Hiyo ni njia nzuri ya kupata vyakula vitamu bure! Inatukumbusha maneno ya mtunga-zaburi: “Jinsi kazi zako zilivyo nyingi, Ee Yehova! Zote umezifanya kwa hekima. Dunia imejaa vitu ulivyotokeza.”—Zaburi 104:24.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 4 Katika makala hii, tunatumia neno “beri” kama inavyoeleweka kwa kawaida kumaanisha tunda lolote dogo laini. Wataalamu wa mimea hutumia neno hilo kumaanisha matunda laini yenye mbegu nyingi. Kupatana na ufafanuzi huo, ndizi na nyanya ni beri.

[Sanduku/ Picha katika ukurasa wa 24, 25]

BILBERRY (Vaccinium myrtillus)

Beri hizo tamu zinazopendwa huitwa pia whortleberry. Mara nyingi beri hizo hutumiwa kutengeneza kitoweo, urojorojo, jemu, au maji ya matunda. Pia hutumiwa kutengeneza vyakula vitamu kama vile keki ya bilberry. Bilberry zilizotoka tu kuchumwa huwa tamu zikiliwa na maziwa. Lakini usile bilberry kwa siri kwa sababu hizo hufanya mdomo uwe na rangi ya bluu. Pia zinaitwa kwa mzaha beri porojo.

[Sanduku/ Picha katika ukurasa wa 25]

CLOUDBERRY (Rubus chamaemorus)

Beri hizi hukua vizuri katika sehemu zisizofikika kwa urahisi kama vile kwenye vinamasi. Zinapatikana zaidi upande wa kaskazini wa Finland. Beri hizo zina maji mengi na lishe kwa sababu zina kiasi kikubwa cha vitamini A na C. Zina vitamini C mara tatu au nne zaidi ya chungwa. Pia ni zenye thamani sana hivi kwamba nyakati nyingine zinaitwa dhahabu inayopatikana kwenye vinamasi. Beri hizo tamu huongeza ladha ya vyakula vinavyoliwa baada ya mlo, nazo pia hutumiwa kutengeneza mvinyo mtamu.

[Hisani]

Reijo Juurinen/Kuvaliiteri

[Sanduku/ Picha katika ukurasa wa 25]

LINGONBERRY (Vaccinium vitis-idaea)

Beri hizo ambazo ni za jamii moja na cranberry, ni maarufu sana nchini Finland na Sweden. Rojo au jeli ya lingonberry ni tamu ikiliwa na milo mingine. Beri hizo za rangi nyekundu nyangavu hutumiwa pia kutengeneza kitoweo, urojorojo, maji ya matunda, na keki. Beri hizo haziozi haraka kwani zina asidi ambazo huzihifadhi. Asidi hizo hufanya beri ziwe na ukakasi kwa hiyo inachukua muda kuzoea ladha yake.

[Sanduku katika ukurasa wa 25]

Si Kazi Inayofurahisha Sikuzote!

Kuchuma beri za msituni ni kazi yenye kupendeza na kuridhisha. * Lakini ina matatizo yake. Pasi na Tuire ni wenzi wa ndoa kutoka Lapland ambao huchuma beri kwa matumizi ya nyumbani na kuuza. Wanasema kwamba wanapochuma beri, nyakati nyingine wao huzungukwa na wadudu wasumbufu kama vile mbu na mainzi. “Wanaudhi sana. Wao huingia machoni na mdomoni,” anasema Tuire. Hata hivyo, unaweza kujilinda kwa kadiri fulani kwa kuvaa nguo zinazofaa na kujipaka dawa ya kufukuza wadudu.

Inaweza kuwa vigumu pia kutembea msituni, hasa unapotembea kwenye maeneo yenye vinamasi. Mahali panapoonekana kuwa imara panaweza kuwa na shimo lenye matope. Pia, Pasi na Tuire wanasema kwamba kuchuma beri kunaweza kuchosha sana. Kuinama na kuchuchumaa kunaweza kusababisha maumivu ya mgongo na miguu.

Si rahisi kupata beri. Pasi anasema, “Unahitaji kutafuta mahali palipo na beri nyingi.” Tuire anaongezea hivi: “Mara nyingi kazi ya kuzitafuta huchosha kuliko kuzichuma.” Pia kusafisha beri baada ya kuzichuma si rahisi.

Kwa sababu ya matatizo hayo, wengine huamua kuwaachia wanyama wa msituni matunda hayo. Lakini bado watu wanaopenda kuchuma beri kama vile Pasi na Tuire, huenda kila mwaka msituni na kwenye vinamasi kutafuta beri. Furaha wanayopata kwa kuchuma beri za msituni ni kubwa kuliko matatizo yoyote wanayokabili.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 27 Si beri zote zinazofaa kuliwa na wanadamu. Nyingine zina sumu. Kabla ya kuchuma beri za msituni, jifunze kutambua zile zinazofaa kuliwa.