Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

▪ Uchunguzi wa hivi karibuni “unaonyesha kwamba Waingereza sita kati ya 10 wanaona kwamba dini inatenganisha watu.”—THE CATHOLIC HERALD, UINGEREZA.

▪ Kituo kikubwa zaidi duniani cha kutokeza umeme kwa kutumia miale ya jua kimejengwa nchini Ureno. Betri zinazotumia nguvu za jua zimeenea katika eneo lenye ukubwa wa ekari 600 na zinaweza kutokeza umeme wa kutosha kwa ajili ya nyumba 30,000 hivi. —EL PAÍS, HISPANIA.

▪ Ulimwenguni pote, vijana 900,000 hufa kila mwaka kutokana na visababishi visivyo vya kiasili—hiyo ni zaidi ya vijana 2,000 kila siku. Visababishi vikubwa ni aksidenti za barabarani, kufa maji, na kuchomeka.—DIE WELT, UJERUMANI.

“Ingawaje kwa ujumla uharibifu wa misitu umepungua katika miaka ya karibuni, bado misitu yenye ukubwa [wa kilomita 200 hivi za mraba] inatoweka kila siku.”—SHIRIKA LA KIMATAIFA LA KILIMO NA CHAKULA LA UMOJA WA MATAIFA, ITALIA.

Mnamo Januari (Mwezi wa 1) 2009, maharamia watano walizama baada tu ya kikundi chao kupokea fidia ya dola 3,000,000 (za Marekani) kutoka katika meli ya mafuta ya Saudia. Mwili wa mmoja wao ulielea hadi ufuoni ukiwa na dola 153,000 mfukoni mwake zilizotiwa ndani ya karatasi ya plastiki. —ASSOCIATED PRESS, SOMALIA.

Vijana Wanaona Kwamba Wanaendekezwa

Kulingana na gazeti de Volkskrant, vijana nchini Uholanzi “wanahisi kwamba rika lao linaendekezwa” na kwamba “wanatiwa moyo sana kujipenda, na hivyo hawawajali wengine.” Kati ya vijana wenye umri wa miaka 16 na 24, vijana “wasiopungua 2 kati ya 3 . . . wanahisi kwamba haki za vijana zinatetewa zaidi kuliko kazi wanazopewa,” linasema gazeti hilo. Maoni ya wengi ni kwamba “vijana wanadai mengi mno . . . na hawajiulizi ni nini wanachoweza kuchangia katika jamii.”

Watoto Wanajitayarishia Chakula

Mwalimu mkuu katika shule moja nchini Japani alipotafuta njia za kuwafanya wazazi na watoto watumie wakati mwingi zaidi pamoja, shule hiyo ilikubali wazo lake la kuwafanya watoto watayarishe mlo mmoja wa mchana kila mwezi. Sasa mamia ya shule zinafanya vivyo hivyo. “Watoto hawatazamiwi wafanye kila kitu wakiwa peke yao,” linasema gazeti IHT Asahi Shimbun la Japani. “Wanafunzi wa kila darasa wanapewa mgawo unaowafaa. Watoto walio katika madarasa ya chini wanasaidiwa na familia zao kupanga orodha ya vyakula watakavyotayarisha pamoja na kununua vyakula hivyo. . . . Wanafunzi katika madarasa ya juu wanajipangia orodha ya vyakula vyenye lishe nzuri.” Matokeo yamekuwaje? “Shule zimeripoti kwamba watoto wameboresha uwezo wao wa kupika, chakula hakitupwi ovyoovyo, na familia zimepata mambo mapya ya kuzungumzia,” linasema gazeti hilo. Pia watoto wanasema kwamba “wamejifunza kuthamini mambo ambayo wazazi wao huwafanyia.”

Kusafisha Eneo la Antaktika

Mwaka uliopita, wataalamu wa Urusi waliondoa takataka zenye uzito wa tani 360 kutoka eneo la Antaktika waliposhiriki katika programu ya pekee ya kusafisha eneo hilo. Takataka zilizotupwa karibu na vituo vya kufanyia utafiti kwenye eneo hilo la Antaktika zinatia ndani vifaa vya ujenzi ambavyo havijatumiwa, mashini zilizoharibika, na mapipa matupu ya mafuta. “Kulingana na sheria za kulinda mazingira ya eneo hilo lililo kwenye ncha ya kusini zaidi ya dunia, kila nchi inapaswa kujiondolea takataka zake,” linaripoti gazeti la Urusi Itogi. “Wajapani ndio wenye bidii zaidi kuondoa takataka zao kwenye eneo hilo.”