Ugonjwa Ulioogopwa Zaidi Katika Karne ya 19
Ugonjwa Ulioogopwa Zaidi Katika Karne ya 19
Ulikuwa mwaka wa 1854, na kwa mara nyingine London ilikumbwa na mlipuko wa kipindupindu—ugonjwa wa tumbo unaomfanya mtu aharishe na kupoteza maji mwilini. Ugonjwa huo ulienea kwa kasi sana. Watu wengi waliokuwa na afya nzuri asubuhi walikuwa wamekufa kufikia usiku. Hakukuwa na tiba.
ULIKUWA ndio ugonjwa wenye kuogopesha katika karne yote, na hakuna aliyejua jinsi ulivyotokea. Wengine walifikiri mtu alipatwa na kipindupindu kwa sababu ya kupumua hewa yenye harufu ya vitu vilivyooza. Huenda makisio yao yakawa yalionekana kuwa yanapatana na akili. Mto Thames, uliopitia London, ulikuwa ukinuka vibaya sana. Je, harufu hiyo mbaya ndiyo iliyosababisha ugonjwa huo?
Miaka mitano mapema, daktari anayeitwa John Snow alikuwa amesema kwamba kipindupindu kinasababishwa, si na hewa chafu, bali maji machafu. Daktari mwingine, William Budd, alisema kwamba kuna kiini fulani kinachofanana na kuvu ambacho kilibeba ugonjwa huo.
Ugonjwa huo ulipolipuka katika mwaka wa 1854, Snow alijaribu kuthibitisha wazo lake kwa kuchunguza maisha ya watu waliopatwa na kipindupindu katika wilaya ya Soho, huko London. ‘Walikuwa wameshiriki katika utendaji gani unaofanana?’ alijiuliza. Uchunguzi wa Snow ulimfanya agundue jambo fulani lenye kushangaza. Wote walioambukizwa kipindupindu katika wilaya hiyo walikuwa wamechota maji ya kunywa katika bomba lilelile, na maji hayo yalikuwa yamechafuliwa na maji-taka yaliyo na kipindupindu! *
Mwaka huohuo hatua nyingine kubwa ya kitiba ilifikiwa wakati mwanasayansi Mwitaliano Filippo Pacini alipochapisha maandishi kuhusu kiini kinachosababisha kipindupindu. Hata hivyo, watu wengi walipuuza uchunguzi wake pamoja na mambo ambayo Snow na Budd walikuwa wamegundua. Kipindupindu kiliendelea kuenea, hadi mwaka wa 1858.
“Uvundo Mkuu”
Bunge halikuwa na haraka ya kujenga mfumo mpya wa kuondoa maji-taka ili kusafisha Mto Thames, lakini joto kali lililotokea katika kiangazi cha mwaka wa 1858 liliwalazimisha wachukue hatua. Uvundo uliotoka katika mto huo uliopita
mbele ya Bunge ulikuwa mkali sana hivi kwamba wanasiasa walilazimika kuweka pazia zilizoloweshwa sabuni ya kuua viini ili kupunguza uvundo huo. Huo, ulioitwa Uvundo Mkuu, uliwasukuma Wabunge wachukue hatua. Katika muda wa siku 18, waliamuru kwamba mfumo mpya wa kuondoa maji-taka ujengwe.Mifereji mikubwa ilijengwa iliyozuia maji-taka yasifike kwenye mto, kisha ikayasafirisha hadi mashariki ya London, ambako mwishowe yaliingia baharini, wakati ambapo maji ya bahari yalijaa. Matokeo yalikuwa yenye kushangaza. Sehemu zote za London zilipounganishwa kwenye mfumo huo mpya, kipindupindu kilikwisha.
Sasa hakukuwa na shaka: Kipindupindu hakikusababishwa na hewa chafu bali kilisababishwa na maji au chakula kichafu. Pia ilikuwa wazi kwamba siri ya kuzuia ugonjwa huo ni kudumisha usafi.
Sheria Iliyotolewa Kabla ya Wakati Wake
Maelfu ya miaka kabla ya kipindupindu kuvamia London, Musa alikuwa ameongoza taifa la Israeli kutoka Misri. Ingawa walitembea katika nyika ya Sinai kwa miaka 40 hivi, Waisraeli hawakukumbwa na magonjwa kama vile kipindupindu. Hilo liliwezekana jinsi gani?
Waisraeli waliagizwa wazike kinyesi cha mwanadamu katika eneo lililo mbali na kambi ili mahali wanapoishi na vyanzo vya maji visichafuliwe. Mwongozo huo uko katika Biblia kwenye Kumbukumbu la Torati 23:12, 13, ambalo linasema:
“Lazima mwe na mahali nje ya kambi ambapo mnaweza kwenda haja. Kati ya vifaa vyenu mtakuwa na jembe, na hilo mtatumia kuchimba shimo na kufunikia mavi yenu.”—“Biblia Habari Njema.”
Mwongozo huo rahisi uliwalinda Waisraeli kutokana na magonjwa yaliyowasumbua watu * Fikiria mfano mmoja.
katika mataifa yaliyowazunguka. Mazoea kama hayo ya kudumisha usafi yameokoa maisha ya watu katika nyakati za kisasa pia.“Hakuna Ugonjwa Mbaya Uliolipuka”
Katika miaka ya 1970, mateso yaliwafanya Mashahidi wengi wa Yehova waondoke nchini Malawi. Walikimbilia nchi jirani ya Msumbiji, ambako wanaume, wanawake, na watoto zaidi ya 30,000 waliishi katika kambi kumi za wakimbizi. Kama inavyojulikana, mara nyingi magonjwa yanayoenezwa kupitia maji husambaa upesi katika kambi za wakimbizi. Kwa hiyo, Mashahidi waliishi jinsi gani chini ya hali hizo?
Lemon Kabwazi, pamoja na wengine 17,000 waliishi katika kambi kubwa zaidi huko Mlangeni. Anakumbuka hivi: “Kambi ilikuwa safi kila wakati. Mashimo ya choo yalichimbwa nje ya kambi, na hakuna mtu aliyeruhusiwa ajichimbie shimo lake ndani ya kambi. Vilevile mashimo ya takataka yalichimbwa mbali na kambi. Wajitoleaji walidumisha usafi katika kila njia, kutia ndani kuhakikisha kwamba maji yaliyochotwa katika visima vilivyochimbwa katika eneo tofauti nje ya kambi yalikuwa safi. Ingawa tulikuwa wengi na tuliishi katika eneo dogo sana, tulidumisha viwango vya Biblia kuhusu usafi, kwa hiyo hakuna ugonjwa mbaya uliolipuka, na hakuna mtu aliyewahi kuugua kipindupindu.”
Kwa kusikitisha, katika maeneo fulani ya ulimwengu, bado kuna nyumba ambazo hazina mifumo inayofaa ya kuondoa maji-taka. Magonjwa yanayosababishwa na kinyesi cha wanadamu husababisha vifo vya watoto 5,000 hivi kila siku.
Ingawa kipindupindu na magonjwa kama hayo yanaweza kuzuiwa, na vilevile jitihada za wanadamu za kudumisha usafi zimetokeza manufaa mengi, Biblia inatoa tumaini kwamba hivi karibuni magonjwa yote yatakomeshwa. Ufunuo 21:4 inasema kwamba chini ya utawala wa Ufalme wa Mungu, “kifo hakitakuwapo tena, wala maombolezo wala kilio wala maumivu hayatakuwapo tena.” Biblia inaahidi hivi kuhusu wakati huo: “Hakuna mkaaji atakayesema: ‘Mimi ni mgonjwa.’”—Isaya 33:24.
Ili ujifunze mengi zaidi kuhusu kile ambacho Ufalme wa Mungu utawafanyia wanadamu, ona sura ya 3 na ya 8 katika kitabu Biblia Inafundisha Nini Hasa? kilichochapishwa na Mashahidi wa Yehova.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 5 Ingawa kufikia mwaka wa 1854 vyoo vya kupiga maji vilikuwa vimebuniwa, mfumo wa kale wa kupitisha maji-taka uliruhusu uchafu wa wanadamu kutiririka kupitia katika mabomba na mifereji hadi ndani ya Mto Thames, uliokuwa chanzo kikuu cha maji ya kunywa.
^ fu. 15 Kwa kuwa kipindupindu husababishwa na chakula au maji yaliyochafuliwa, siri ya kuzuia ugonjwa huo ni kuchunga chochote kinachoingia kupitia mdomo. Kuua viini katika maji na kupika chakula kabisa ni njia muhimu za kujilinda.
[Blabu katika ukurasa wa 21]
Mto Thames ulipita katikati ya London na ulikuwa na maji-taka yaliyobeba kipindupindu, kama inavyoonyeshwa katika picha nyingi za wakati huo
[Picha katika ukurasa wa 22]
Huko Msumbiji, wanaume, wanawake, na watoto zaidi ya 30,000 waliishi katika kambi kumi za wakimbizi ambazo zilidumishwa zikiwa safi
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 20]
Death on Thames: © Mary Evans Picture Library; map: University of Texas Libraries