Retina Iliyo Juu Chini
Je, Ni Kazi ya Ubuni?
Retina Iliyo Juu Chini
● Jicho la mwanadamu lina retina ambayo ni utando ulio na chembe milioni 120 hivi zinazoitwa vipokezi-mwanga, ambavyo hufyonza miale ya jua na kuibadilisha kuwa mawimbi ya umeme. Ubongo wako hugeuza mawimbi hayo kuwa picha. Wanamageuzi wanadai kwamba mahali ambapo retina ipo katika macho ya viumbe wenye uti wa mgongo inaonyesha kwamba jicho halikubuniwa.
Fikiria hili: Retina ya viumbe wenye uti wa mgongo iko juu chini na hivyo kufanya vipokezi-mwanga viwe nyuma ya retina. Ili mwangaza ufikie chembe hizo, ni lazima upitie matabaka kadhaa ya chembe. Mwanabiolojia wa mageuzi Kenneth Miller anasema hivi, “mfumo huu hugawanya mwangaza na kufanya macho yachuje habari ambayo hatuhitaji kuona.”
Kwa sababu hiyo, wanamageuzi wanadai kwamba retina iliyo juu chini ni uthibitisho wa kutosha wa kazi duni isiyo na ubuni wowote. Mwanasayansi mmoja alisema kwamba “ni upumbavu [kwa retina] kuwa juu chini.” Hata hivyo, utafiti zaidi unaonyesha kwamba chembe hizo za retina iliyo juu chini zimepangwa vizuri sana kando ya tishu inayoitwa epitheliamu ambayo ni tabaka la chembe zinazoandaa oksijeni pamoja na virutubisho vinavyohitajika sana ili jicho lione vizuri. Mwanabiolojia Jerry Bergman, pamoja na mtaalamu wa macho Joseph Calkins waliandika kwamba “ikiwa epitheliamu ingekuwa mbele ya retina, basi mtu hangeweza kuona vizuri.”
Retina iliyo juu chini ina manufaa zaidi kwa viumbe wenye uti wa mgongo walio na macho madogo. Profesa Ronald Kröger wa Chuo Kikuu cha Lund, Sweden anasema hivi: “Ili jicho liweze kuona picha zilizo dhahiri, ni lazima kuwe na nafasi kati ya lenzi ya jicho na zile chembe zinazoitwa vipokezi-mwanga. Chembe za neva zinapojaa kwenye nafasi hiyo, inaonyesha kwamba wanyama hao hawajapoteza nafasi hiyo.”
Isitoshe, chembe za neva zinapokuwa zimejipanga vizuri karibu na vile vipokezi-mwanga, habari inayonaswa na jicho hupokewa na kukaguliwa upesi na inategemeka.
Una maoni gani? Je, retina iliyo juu chini ni kitu hafifu kilichojitokeza chenyewe? Au iliumbwa?
[Mchoro katika ukurasa wa 15]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Vipokezi-mwanga
Mwangaza
Tishu ya epitheliamu
Mwangaza
Retina
Neva kuu ya jicho