Shahamu ya Wanyama wa Baharini
Je, Ni Kazi ya Ubuni?
Shahamu ya Wanyama wa Baharini
● Kwa miaka mingi wanasayansi hawakuweza kuelewa jinsi pomboo wanavyoweza kuogelea kwa mwendo wa kilomita 40 kwa saa. Wanasayansi walifikiria kwamba wanyama hao hawana misuli yenye nguvu kuwawezesha kusonga kwa kasi hivyo. Lakini sababu moja inayowawezesha pomboo kufanya hivyo ni shahamu yao, tishu fulani tata yenye mafuta mengi ambayo pia inapatikana ndani ya ngozi ya pomboo fulani wasioonekana mara nyingi, nyangumi, na wanyama wengine wa baharini.
Fikiria hili: “Shahamu ni tabaka nene la tishu iliyopangwa kwa utaratibu sana iliyo na chembe nyingi za mafuta,” kinasema kitabu New World Encyclopedia. Shahamu hufunika mwili wote wa mnyama, na “imeunganishwa kwa nguvu sana kwenye misuli na mifupa yote kupitia mitandao ya kano zilizopangwa kwa utaratibu wa hali ya juu sana.” Mitandao hiyo imefanyizwa kwa nyuzinyuzi zinazoweza kutanuka na kolagini, ambayo ni protini inayopatikana pia katika ngozi na mifupa. Kwa hiyo, shahamu si mafuta tu yanayohifadhi joto mwilini. Ni muungano wa tishu mbalimbali za hali ya juu na zilizo hai.
Hata hivyo, ni kwa njia gani shahamu inasaidia pomboo waogelee haraka hivyo—pomboo wa Dall wakisonga kwa mwendo unaofikia kilomita 56 kwa saa? Sababu moja ni kwamba shahamu inawasaidia wanyama kuwa na umbo lililonyooka. Sababu nyingine ni kwamba shahamu iliyo katikati ya sehemu za mkia na pezi la mgongoni ina kolagini na nyuzinyuzi zinazoweza kutanuka zilizoingiana, jambo linalosaidia mkia uweze kujipinda na kuhifadhi nishati. Kwa hiyo, misuli inaposogeza mkia upande mmoja, shahamu inayotenda kama springi huuvuta mkia na hivyo kusaidia kumsukuma mnyama na kwa hiyo anatumia nishati kidogo.
Pia, shahamu husaidia katika kuelea na kuhifadhi joto. Mafuta yaliyo katika shahamu huhifadhi nishati kwa ajili ya wakati ambapo mnyama hawezi kupata chakula cha kutosha. Si ajabu kwamba wale wanaojaribu kuboresha uwezo wa vyombo vya baharini na uwezo wake wa kusonga wamependezwa kuchunguza jinsi shahamu inavyotenda kazi.
Una maoni gani? Je, shahamu iliyo na uwezo mwingi wenye kustaajabisha, ilijitokeza yenyewe? Au ilibuniwa?
[Mchoro katika ukurasa wa 17]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Nyuzi mojamoja
Kolagini na nyuzinyuzi zinazoweza kutanuka zilizoingiana