Jiji la Kipekee Lililojengwa kwa Karatasi
Jiji la Kipekee Lililojengwa kwa Karatasi
‘E TI jiji lililojengwa kwa karatasi?’ huenda ukauliza. Ndiyo, lakini si jiji halisi bali ni mfano wa jiji hilo. Jiji hilo ni Prague, mji mkuu wa Jamhuri ya Cheki, na mfano wa jiji hilo umehifadhiwa katika Jumba la Makumbusho la Manispaa ya Prague. Mfano huo ulijengwa na Antonín Langweil kwa miaka 11, kuanzia 1826 hadi 1837, mwaka ambao alikufa. Ni nini kilichomchochea Langweil aanzishe mradi huo mgumu?
Langweil alizaliwa mwaka wa 1791 katika mji wa Postoloprty katika eneo linalojulikana leo kama Jamhuri ya Cheki. Baada ya kusomea lithografia (sanaa ya kupachika michoro iliyotiwa rangi kwenye mwamba) katika Chuo cha Sanaa cha Vienna, Austria, alifungua kiwanda cha kwanza cha lithografia huko Prague. Ingawa alikuwa msanii mzuri, hakufanikiwa katika biashara hiyo, na kiwanda chake kikafilisika. Mnamo 1826, alipokuwa akihudhuria maonyesho fulani huko Prague, aliona mfano wa jiji la Paris, Ufaransa uliotengenezwa kwa plasta. Akichochewa na mfano huo, Langweil aliamua kutengeneza mfano wa jiji la Prague akitumia katoni ngumu na mbao chache.
Lakini kwanza Langweil alitumia miaka mingi akichunguza kwa makini jiji la Prague. Alitembea katika barabara zote, akichora na kuandika mahali ambapo kila jengo lilikuwa, kila benchi kwenye bustani, kila kibanda, kila sanamu, na kila mti ulipokuwa. Hata alichora
mapipa yaliyokuwa chini, madirisha yaliyovunjika, ngazi iliyoegemea ukutani, na marundo ya mbao! Kisha akaanza kutengeneza mfano huo kwa kutumia vipimo vilivyopunguzwa kwa uwiano wa 1 kwa 480. Ili kuongezea mapato yake madogo, alitengeneza pia mifano ya nyumba za matajiri.Katika mwaka wa 1837, Langweil aliugua kifua kikuu na kufa mwezi wa Juni mwaka huo, akaacha mke na binti watano. Miaka mitatu baada ya kifo chake, mfano aliotengeneza uliwekwa katika Jumba la Makumbusho la Uzalendo, ambalo sasa linaitwa Jumba la Makumbusho la Kitaifa. Ulifikaje huko? Mnamo 1840, mjane wa Langweil alimwomba Maliki Ferdinand wa Kwanza anunue mfano huo, naye akaununua na kuutoa kama mchango kwa jumba ambalo leo ni jumba la makumbusho la kitaifa la Jamhuri ya Cheki. Ulisafirishwa ndani ya masanduku tisa. Baadaye, msemaji wa Jumba la Makumbusho la Jiji la Prague, ambako mfano huo umehifadhiwa leo, alisema hivi: “Mfano uliotengenezwa na Langweil ulionekana kwenye maonyesho mara chache sana katika karne ya 19. Katika mwaka wa 1891, ulikuwa mojawapo ya vitu vilivyoonyeshwa katika Maonyesho ya Kitaifa ya Jubilee. Ili mfano huo uwekwe kwenye maonyesho hayo, ulifanyiwa marekebisho yaliyogharimu pesa nyingi . . . Kuanzia mwaka wa 1905, mfano huo uliwekwa kwenye sehemu ambapo nguzo za mawe na vitu vilivyochimbuliwa huwekwa katika Jumba la Makumbusho la Kitaifa.”
Kivutio kwa Wanahistoria
Mfano wa Langweil uliotengenezwa kwa karatasi ni maarufu sana. Una urefu wa mita 5.76 na upana wa mita 3.24, na umefungiwa katika sanduku la kioo huku ukimulikwa kwa taa nyingi ndogo ambazo zinaning’inia ndani ya sanduku hilo. Mfano huo huonekana kuwa halisi sana hivi kwamba lazima mtu ajikumbushe kwamba anatazama kitu kilichotengenezwa kwa karatasi! Langweil alijenga kila moja ya majengo zaidi ya elfu mbili kwa usahihi kabisa.
Kwa mfano, Langweil alilipatia kila jengo nambari ya usajili. Pia aliweka taa za barabarani, mitaro, na barabara zilizojengwa kwa mawe. Alijenga makanisa yakiwa na madirisha yaliyopakwa rangi, kutia ndani madirisha ambayo hayakuwa na vioo au vioo vilivyokuwa vimevunjika. Mfano huo pia ulionyesha nyumba zote ambazo plasta ilikuwa imebambuka na matofali yalikuwa yakionekana. Pia alijenga Mto Vltava ambao hupitia Prague.
Leo, mfano huo wa karatasi uliotengenezwa na Langweil ni kitu cha kale chenye kupendeza na pia kivutio kwa watu wanaopenda sanaa na pia wanahistoria ambao wanataka kuona jinsi jiji la Prague limebadilika kadiri miaka imepita. Kwa kweli mfano huo wa Prague ni tofauti na jinsi jiji hilo lilivyo leo kwa sababu baadhi ya majengo yamejengwa upya au kurekebishwa, hasa sehemu ambako Wayahudi waliishi na sehemu inayoitwa Mji wa Kale. Kwa sababu ya teknolojia ya kisasa, wageni wanaweza kuona mfano huo wa jiji la Prague katika mwaka wa 1837 uliotengenezwa na Langweil kwenye kompyuta.
Mnamo Aprili 1837, Langweil aliyekuwa akiugua aliomba kwamba mfano wake uwekwe kwenye Jumba la Makumbusho la Uzalendo kama lilivyoitwa wakati huo, lakini wasimamizi wa jumba hilo walikataa ombi lake. Lazima hilo liwe lilimvunja moyo sana! Lakini hebu wazia kama angetembelea jumba hilo leo na kuona mfano aliotengeneza wa jiji la kale la Prague kwenye kompyuta. Bila shaka, angeona kwamba jitihada zake kubwa hazikuwa za bure.
[Picha katika ukurasa wa 10]
Antonín Langweil
[Picha katika ukurasa wa 10]
Mfano wa jiji la Prague ambao Langweil alitengeneza kwa karatasi
[Picha katika ukurasa wa 10, 11]
Picha ya karibu ya jiji la karatasi lililotengenezwa na Langweil
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 10]
Page 10, Langweil: S laskavým svolením Národního muzea v Praze; pages 10 and 11, model photos: S laskavým svolením Muzea hlavního mesta Prahy