Kuutazama Ulimwengu
Nchini Ujerumani, karibu asilimia 33 ya watoto waliozaliwa mwaka wa 2010, walizaliwa nje ya ndoa, ikilinganishwa na asilimia 15 katika mwaka wa 1993.—ÄRZTE ZEITUNG na THE LOCAL, UJERUMANI.
Kulingana na takwimu za sensa ya mwaka wa 2010, asilimia 69.4 ya watoto nchini Marekani wanaishi na wazazi wote wawili, asilimia 23.1 wanaishi na mama pekee, asilimia 3.4 wanaishi na baba pekee, na asilimia 4.1 hawaishi na mzazi yeyote.—IDARA YA SENSA, MAREKANI.
Misiba ya asili iligharimu uchumi wa ulimwengu kiasi cha dola bilioni 380 hivi (za Marekani) katika mwaka wa 2011. Tetemeko la nchi lililoikumba Japani ndilo lililokuwa “lenye gharama kubwa kuliko msiba wowote wa asili uliopata kutokea, lilisababisha hasara ya dola bilioni 210—bila kutia ndani hasara ya mkasa wa nyuklia huko Fukushima.”—GAZETI NEW SCIENTIST, UINGEREZA.
Duniani pote, chakula ambacho huibwa mara nyingi ni jibini. Zaidi ya asilimia 3 ya jibini inayouzwa kwenye maduka ya rejareja ulimwenguni pote huibwa na wateja na wafanyakazi wa maduka hayo.—KITUO CHA UTAFITI WA UCHUUZI WA REJAREJA, UINGEREZA.
Madhara ya Kupiga Mpira kwa Kichwa
Katika mchezo wa soka, kupiga mpira kwa kutumia kichwa ni sehemu ya mchezo. Hata hivyo, uchunguzi wa hivi karibuni kwa kutumia eksirei za hali ya juu na kuchunguza uwezo wa akili umeibua maswali kuhusu usalama wa kupiga mpira kwa kichwa kwa muda mrefu. Kulingana na watafiti kwenye Chuo cha Tiba cha Albert Einstein, huko New York, Marekani, zoea hilo “huongeza hatari ya kupatwa na majeraha kwenye ubongo na kuathiri uwezo wa akili wa kufikiri.” Majeraha yaligunduliwa miongoni mwa wachezaji wasio na uzoefu ambao walipiga mpira kwa kichwa zaidi ya mara 1,000 hadi 1,500 hivi kwa mwaka, lakini kiwango hicho kinalingana na “mara ambazo mchezaji wa kawaida hupiga mpira kwa kichwa kila siku.”
Magari Yasiyotoa Sauti Ni Hatari kwa Wapita Njia
“Watu wanaotetea haki za wapita-njia, wana wasiwasi kuhusu usalama wa magari yanayotumia umeme na wakati uleule petroli,” inasema taarifa kutoka kwa Wizara ya Usafiri ya Marekani. “Wasiwasi wao ni kwamba magari hayo hayana kelele, kwa hiyo wapita-njia na waendesha baiskeli hawawezi kujua ikiwa kuna gari barabarani au wanapokaribia makutano ya barabara.” Ripoti hiyo inasema kwamba “kuna uwezekano mkubwa wa magari hayo yasiyotoa sauti kuwagonga wapita-njia” kuliko magari ya kawaida. Shirika la Kitaifa la Marekani la Usimamizi wa Usalama Barabarani limependekeza kwamba magari hayo yarekebishwe ili yaweze kutokeza sauti yanapokuwa kwenye mwendo wa taratibu.