Caucasus “Mlima Wenye Lugha Nyingi”
HEBU wazia unajikuta katika eneo lenye milima mingi lililo na ukubwa unaokaribia kulingana na nchi ya Hispania. Unagundua kuwa eneo hilo lina mataifa mengi, na kila taifa lina lugha yake. Katika baadhi ya maeneo, hata watu wanaoishi katika vijiji jirani hawaelewi lugha ya wenzao! Hata wanajiografia wa enzi za kati walishangazwa pia, hivi kwamba mmoja wao akalifafanua eneo la Caucasus kuwa “mlima wenye lugha nyingi.”
Eneo la Caucasus liko kati ya Bahari Nyeusi na Bahari ya Kaspiani, na kwa sababu hiyo liko kati ya mabara mawili na ustaarabu mbalimbali jambo ambalo limesaidia eneo hilo kuwa na aina mbalimbali za utamaduni na historia ndefu. Watu wa eneo hilo wanajulikana kwa kuheshimu watu wenye umri mkubwa, kupenda kucheza dansi, na kwa ukarimu wao. Lakini jambo linalowastaajabisha zaidi wageni ni unamna-namna wa vikundi vya kikabila na lugha—kwa kweli eneo hilo lina lugha nyingi zaidi kuliko maeneo yote ya Ulaya yenye ukubwa unaolingana nalo.
Unamna-namna Wenye Kushangaza
Katika karne ya tano K.W.K., mwanahistoria Mgiriki Herodoto aliandika hivi: “Watu wa mataifa mbalimbali wanaishi katika eneo la Caucasus.” Karibu mwanzoni mwa karne ya kwanza W.K., mwanafalsafa mwingine Mgiriki anayeitwa Strabo aliandika kuhusu makabila 70 ya eneo hilo. Kila kabila lilikuwa na lugha yake, na yote yalikuja kufanya biashara katika jiji la Dioscurias, eneo ambalo sasa kuna jiji la kisasa la Sukhumi, kwenye pwani ya Bahari Nyeusi. Miaka mingi baadaye, Plini Mkubwa, aliyekuwa msomi Mroma, aliandika kwamba Waroma walihitaji watafsiri wapatao 130 ili waweze kufanya biashara katika jiji la Dioscurias.
Leo bado kuna zaidi ya vikundi 50 vya makabila ambavyo vinaishi katika eneo la Caucasus. Kila kikundi kina desturi zake na mara nyingi kila kikundi kina aina yake yenyewe ya mavazi, sanaa, na ujenzi. Kuna angalau lugha 37 za kiasili katika eneo hilo, na baadhi ya lugha hizo zinazungumzwa na mamilioni ya watu, lakini nyingine zinazungumzwa katika vijiji fulani tu. Jamhuri ya Dagestan iliyo upande wa Urusi ndilo eneo lenye lugha nyingi zaidi, kwani karibu makabila 30 yanaishi katika eneo hilo. Mpaka sasa wataalamu wa lugha hawajui
jinsi lugha hizo zinavyohusiana wala jinsi zilivyotokea.Je, ungependa kuona jinsi maandishi ya eneo la Caucasus yalivyo? Tovuti rasmi ya Mashahidi wa Yehova,www.mr1310.com/sw, ina machapisho ya lugha zaidi ya 400. Miongoni mwa lugha hizo kuna lugha kadhaa ambazo huzungumzwa katika eneo la Caucasus, eneo lenye kuvutia ambalo kwa kufaa linaitwa “mlima wenye lugha nyingi.”