Mambo Unayopaswa Kujua Kuhusu Kifafa
RAFIKI yako anaanguka chini na kupoteza fahamu. Mwili wake unakakamaa, kisha unaanza kusukasuka. Ukijua kwamba mtu huyo ana kifafa, huenda ukampa huduma ya kwanza. Hebu tuone mambo kadhaa ya msingi kuhusu ugonjwa huu ambao mara nyingi haueleweki.
Kifafa ni nini? Kifafa ni ugonjwa wa ubongo unaomfanya mtu azimie. Huenda mtu akazimia kwa dakika tano hivi. Kisa kama kile kilichotajwa katika fungu linalotangulia kinaonyesha aina ya kifafa inayoitwa kifafa kikuu.
Ni nini humfanya mtu azimie? Watafiti wanasema kwamba mtu huzimia kunapokuwa na utendaji usio wa kawaida katika chembe za ubongo. Haieleweki ni kwa nini utendaji huo hutukia.
Ninapaswa kufanya nini nikimwona mtu akipatwa na kifafa kikuu? Tovuti ya Kenya inayoitwa The Beehive inaorodhesha mambo unayopaswa kufanya: ‘Usijaribu kumzuia kwa kutumia nguvu. Kufanya hivyo kunaweza kusababisha majeraha kwa mgonjwa na pia kwa yule anayejaribu kumsaidia. Kusukasuka kunapoanza kupungua, hakikisha ya kwamba kupumua kumerudia hali yake ya kawaida.’ Tovuti hiyo pia inasema: “Ikiwa kuzirai kumekaa zaidi ya dakika 5, mpeleke mgonjwa hospitalini. Hili huwa nadra lakini lifanyikapo huwa hatari sana na ni lazima umkimbize mgonjwa hospitalini hata ikiwa bado yuko katika hali hiyo ili kuokoa maisha yake.” Inasema pia unapaswa kumpeleka hospitalini “ikiwa kuzirai kutaisha na kujirudia tena mara hiyo hiyo kabla ya mgonjwa kupata nafuu.”
Ninaweza kumsaidiaje mgonjwa anapozimia? Weka kitu laini kati ya kichwa chake na sakafu, na uondoe vitu vyote vyenye ncha kali vilivyo karibu na kichwa chake. Mwili wake unapoacha kusukasuka, mgeuze alalie ubavu wake kama picha kwenye ukurasa unaofuata inavyoonyesha.
Nifanye nini mgonjwa anapopata fahamu? Kwanza, mhakikishie kwamba yuko salama. Kisha msaidie asimame wima na umwongoze hadi mahali anapoweza kupumzika kabisa. Watu wengi huwa wamechanganyikiwa na wanahisi usingizi baada ya kuzimia; wengine hupona upesi na wanaweza kuendelea kufanya kazi waliyokuwa wakifanya kabla ya tukio hilo.
Je, watu wote wanaoshikwa na kifafa husukasuka? La. Wagonjwa fulani hupoteza fahamu kwa muda mfupi sana bila hata kuanguka chini. Aina hiyo ya kifafa inaitwa kifafa kidogo, na mgonjwa haathiriki kwa muda mrefu. Watu fulani wanaoshikwa na aina hiyo ya kifafa wanaweza kupoteza fahamu kwa muda wa dakika kadhaa. Hilo linapotokea, mgonjwa anaweza kutembea huku na huku ndani ya chumba, avute kwa nguvu mavazi yake, au atende kwa njia ya isiyo ya kawaida. Baada ya tukio hilo, huenda akahisi kizunguzungu.
Watu wenye kifafa huhisije? Watu wengi walio na kifafa huwa na hofu kila wakati kwa kuwa hawajui ugonjwa huo utawashika tena lini na utawashikia wapi. Ili kuepuka aibu, huenda wakaepuka kuwa mahali palipo na watu.
Ninaweza kumsaidiaje mtu aliye na kifafa? Mtie moyo aeleze hisia zake. Sikiliza kwa makini. Mwulize angependa umsaidiaje anaposhikwa na kifafa. Kwa kuwa watu wengi walio na ugonjwa huo hawaendeshi gari, huenda ukajitolea kumbeba kwenye gari lako au unaweza kumsaidia kununua vitu na kumfanyia shughuli mbalimbali.
Je, mtu anaweza kupunguza au kuzuia mara anazozimia? Hali fulani huchangia kuzimia, kama vile kuwa na mkazo au kukosa usingizi. Kwa sababu hiyo, wataalamu wanawatia moyo watu walio na ugonjwa huo wapumzike vya kutosha na wafanye mazoezi kwa ukawaida ili wapunguze mkazo. Katika visa fulani, dawa zimewasaidia wagonjwa wasizimie.