Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Marekani

Uchunguzi mmoja ulionyesha kwamba asilimia 33 hivi ya watu waliokuwa wakitembea kwa miguu walikengeushwa walipokuwa wakivuka barabara zenye shughuli nyingi—kwa sababu walikuwa wakisikiliza muziki, wakiongea kwenye simu na kufanya mambo mengine. Kikengeusha fikira hatari zaidi kilikuwa ni kutuma ujumbe mfupi. Watu waliokuwa wakituma ujumbe walichukua muda mrefu zaidi kuvuka barabara, wengi wao hawakutii taa za barabarani, walivukia mahali pasipofaa, au bila kuangalia pande zote mbili za barabara.

Nigeria

Wanawake kutoka Nigeria wanaosafirishwa Ulaya na watu wanaofanya biashara ya kuuza watu hulazimishwa kula kiapo cha kutunza siri katika mahekalu ya wachawi. Ili kuwadhibiti wanawake hao na kuhakikisha kwamba wanatii wakiwa watumwa wa ngono, wafanya-biashara hao huwatisha kwamba wataadhibiwa na roho waovu.

Hispania

Kati ya asilimia 5 na 10 ya watu ambao wamekaa muda mrefu bila kuajiriwa huondoa habari kuhusu shahada za chuo kikuu na habari za ujuzi wao wanapotuma maombi ya kazi kwa sababu habari hizo zinawafanya waonekane wanastahili mshahara mkubwa kuliko kazi wanayotafuta.

ULIMWENGU

Moshi unaotokezwa na majiko ya kuni au mkaa unaonwa kuwa ndio kisababishi kikubwa cha vifo katika nchi zinazoendelea. Katika nchi hizo, watu milioni nne hufa kila mwaka kutokana na magonjwa ya mfumo wa kupumua yanayosababishwa na moshi. Watafiti wanasema kwamba kemikali zenye sumu zinazotolewa na majiko hayo ni hatari kama sumu iliyo katika moshi wa sigara.