Je, Unakabili Hatari ya Kupata—Ugonjwa wa Fizi?
UGONJWA huu unawapata watu wengi sana ulimwenguni. Hata hivyo, katika hatua za kwanza dalili zake hazionekani haraka. Ugonjwa wa fizi ni hatari kwa kuwa hautambuliki mapema. Kitabu International Dental Journal kinataja ugonjwa wa fizi kati ya magonjwa ya kinywa yanayosababisha “tatizo kubwa la afya ya umma.” Kinaendelea kusema kwamba ugonjwa wa kinywa “unaweza kusababisha uchungu mwingi na kuteseka na vilevile kupunguza uwezo wa mtu wa kula na kufurahia maisha.” Kuchunguza ugonjwa huo kunaweza kukusaidia kujikinga.
Taarifa Kuhusu Ugonjwa wa Fizi
Ugonjwa wa fizi una hatua mbalimbali. Hatua ya kwanza ni kuvimba fizi (gingivitis). Fizi zinazotoa damu ni dalili ya hatua hiyo. Huenda mtu akatokwa na damu anapopiga mswaki, au anapotoa uchafu kwenye meno kwa kutumia uzi mwembamba au bila sababu yoyote. Vilevile, kutokwa na damu mtu anapochunguzwa meno na daktari ni dalili ya ugonjwa huo.
Ugonjwa wa fizi husonga kwenye hatua inayofuata (periodontitis). Kufikia hatua hiyo, mifupa na fizi zinazotegemeza meno, huanza kuharibika. Ugonjwa huo wa fizi huenda usiwe na dalili zozote hadi unapokuwa mbaya zaidi. Dalili fulani za hatua hiyo ni kutokea kwa nafasi kati ya fizi na meno; kulegea kwa meno; mianya kati ya meno; kunuka mdomo; fizi zinazoachana na meno na kufanya meno yaonekane kuwa marefu zaidi; na kutokwa na damu kwenye fizi.
Chanzo na Madhara ya Ugonjwa wa Fizi
Kuna mambo kadhaa yanayochangia kupata ugonjwa wa fizi. Utando wa bakteria ambao kwa kawaida hutokea kwenye meno ndicho chanzo kikuu. Usipotolewa, bakteria husababisha kuvimba kwa fizi. Hatua hiyo inapoendelea, fizi huachana na meno, na hivyo utando huo wa bakteria husambaa na kuingia chini ya fizi. Bakteria zinapofikia hatua hiyo, uvimbe huendelea kuharibu mifupa na fizi. Utando huo, iwe uko juu au chini ya fizi, unaweza kuwa mgumu na kuwa ukoga. Ukoga pia una bakteria, na kwa kuwa ni mgumu na hushikamana na meno, hauwezi kutolewa kwa urahisi kama utando. Hivyo, bakteria huendelea kuharibu fizi.
Kuna mambo mengine pia yanayochangia ugonjwa wa fizi. Yanatia ndani uchafu mdomoni, madawa yanayopunguza kinga mwilini, magonjwa yanayosababishwa na virusi, mkazo, kisukari, kunywa pombe kupita kiasi, kutumia tumbaku, na mabadiliko ya homoni kwa sababu ya mimba.
Ugonjwa wa fizi unaweza kukuathiri kwa njia nyingine pia. Maumivu mdomoni na kung’oka meno kunaweza kupunguza uwezo wako wa kutafuna chakula na kukifurahia. Pia, unaweza kuathiri matamshi na sura yako. Vilevile utafiti umeonyesha kwamba usafi mdomoni unahusiana na afya ya mtu kwa ujumla.
Kutambua na Kutibu Ugonjwa wa Fizi
Unawezaje kujua kama una ugonjwa wa fizi? Huenda ukaona baadhi ya dalili zilizotajwa kwenye makala hii. Ukiziona ni vizuri kumwona daktari maalumu wa meno ili achunguze fizi zako.
Je, ugonjwa wa fizi unaweza kutibiwa? Inawezekana kuutibu katika hatua za kwanza. Ugonjwa wa fizi unapoenea sana, basi lengo ni kuuthibiti ili usiendelee kuharibu mifupa na fizi zinazotegemeza meno. Madaktari wa meno hutumia vifaa vya pekee vinavyoweza kuondoa utando na ukoga kwenye meno, iwe ni chini au juu ya fizi.
Hata ikiwa si rahisi kwako kupata matibabu ya meno, unaweza kuzuia ugonjwa huo hatari usikupate. Kusafisha mdomo vizuri na kwa ukawaida ndiyo njia bora zaidi ya kuzuia ugonjwa wa fizi.