Kuhani Mkuu Aliyemhukumu Yesu
Kuhani Mkuu Aliyemhukumu Yesu
KATIKA Novemba 1990, watu waliokuwa wakitengeneza bustani na barabara kilometa moja hivi kusini mwa Jiji la Kale la Yerusalemu walifanya uvumbuzi wenye kustaajabisha. Kwa ghafula, trekta moja iliporomosha dari la pango fulani la kale la kuzikia. Eneo lililokuwa na pango hilo lilitumiwa kuzikia kuanzia karne ya kwanza K.W.K. hadi karne ya kwanza W.K. Uvumbuzi uliofanywa ndani ya pango hilo ulistaajabisha sana.
Pango hilo lilikuwa na masanduku 12 ya mifupa, na mifupa ya watu waliokufa ilikuwa imeingizwa ndani ya masanduku hayo baada ya kukaa makaburini kwa mwaka mmoja hivi na minofu kuoza. Kando ya sanduku moja lililokuwa limechongwa vizuri ambalo linasemekana kuwa mojawapo ya masanduku bora zaidi kuwahi kupatikana, kulikuwa na jina Yehosef bar Caiapha (Yosefu mwana wa Kayafa).
Uthibitisho unaonyesha kwamba huenda hilo ndilo kaburi la kuhani mkuu aliyesimamia kesi muhimu zaidi kuwahi kufanywa katika mahakama, yaani, ile ya Yesu Kristo. Mwanahistoria Myahudi Yosefo anamtaja kuhani huyo mkuu kuwa “Yosefu, aliyeitwa Kayafa.” Katika Maandiko, anaitwa tu Kayafa. Kwa nini tupendezwe na habari zake? Ni nini kilichomchochea kumhukumu Yesu?
Familia na Malezi
Kayafa alioa binti ya Anasi, kuhani mwingine mkuu. (Yohana 18:13) Huenda mapatano hayo ya ndoa yalifanywa miaka mingi kabla ya arusi, kwa kuwa huenda familia zote mbili zilitaka kuhakikisha kwamba zinafanya mapatano yanayofaa. Hilo lilimaanisha kuchunguza rekodi za ukoo ili kuhakikisha kwamba ukoo wa kikuhani ulidumishwa ukiwa safi. Inaonekana familia zote mbili zilikuwa tajiri na za hali ya juu, na huenda zilipata utajiri huo kutokana na mali nyingi ambazo zilimiliki huko Yerusalemu. Hapana shaka kwamba Anasi alitaka kuhakikisha kwamba mwana-mkwe wake wa wakati ujao atakuwa mshiriki wake wa kisiasa mwenye kutegemeka. Inaonekana kwamba Anasi na Kayafa walikuwa washiriki wa madhehebu yenye uwezo mkubwa ya Masadukayo.—Matendo 5:17.
Kwa sababu alikuwa mshiriki wa familia mashuhuri ya kikuhani, huenda Kayafa alielimishwa katika Maandiko ya Kiebrania na fasiri yake. Huenda utumishi wake hekaluni ulianza alipokuwa na umri wa miaka 20, lakini haijulikani alikuwa kuhani mkuu akiwa na umri gani.
Makuhani Wakuu na Wakuu wa Makuhani
Mwanzoni cheo cha kuhani mkuu kilipatikana kupitia urithi, na mtu angedumu katika cheo hicho hadi kifo. Lakini katika karne ya pili K.W.K., Wahasmoni walinyakua cheo cha kuhani mkuu. * Herode Mkuu aliwaweka rasmi na kuwaondoa makuhani wakuu, hivyo akaonyesha wazi kwamba yeye ndiye aliyesimamia uteuzi wa kuhani mkuu. Magavana Waroma walifanya hivyo pia.
Mambo hayo yalisababisha kutokezwa kwa kikundi cha “wakuu wa makuhani” kinachotajwa katika Maandiko. (Mathayo 26:3, 4) Zaidi ya Kayafa, kikundi hicho kilitia ndani makuhani wakuu wa zamani, kama vile Anasi, ambaye aliondolewa katika cheo chake lakini akaendelea kukishikilia. Kikundi hicho kilitia ndani pia watu wa ukoo wa karibu wa makuhani wakuu wa wakati huo na wa zamani.
Waroma waliruhusu Wayahudi wa tabaka la juu, waliotia ndani wakuu wa makuhani, wasimamie mambo huko Yudea. Hilo liliiwezesha Roma kudhibiti mkoa huo na kujipatia mapato ya kodi bila kutuma wanajeshi wengi huko. Roma ilitazamia Wayahudi wenye mamlaka wadumishe utaratibu na kulinda masilahi yake. Magavana wa Roma hawakuwapenda viongozi wa kidini wa Wayahudi, ambao walichukia kutawaliwa na Roma. Lakini wote wangefaidika kwa kushirikiana ili kudumisha serikali imara.
Kufikia wakati wa Kayafa, kuhani mkuu ndiye aliyekuwa kiongozi wa kisiasa wa Wayahudi. Anasi alipewa cheo hicho na Kirenio, gavana Mroma wa Siria, katika mwaka wa 6 au wa 7 W.K. Mapokeo ya Marabi yanaonyesha kwamba familia za Wayahudi za tabaka la juu zilijulikana hasa kwa pupa, kupendelea watu wa familia, uonevu, na jeuri. Mwandishi mmoja anadai kwamba kwa kuwa Anasi alikuwa kuhani mkuu, huenda angehakikisha kwamba mwana-mkwe wake “amepandishwa cheo cha ukuhani haraka; kwa sababu ikiwa Kayafa angekuwa na cheo cha juu, basi angemfaidi sana Anasi.”
Valerio Grato, gavana wa Yudea, alimwondoa Anasi katika cheo hicho yapata mwaka wa 15 W.K. Watu wengine watatu, kutia ndani mwana mmoja wa Anasi, walitumikia wakiwa makuhani wakuu kwa muda mfupi wakifuatana. Kayafa alipata cheo cha kuhani mkuu yapata mwaka wa 18 W.K. Pontio Pilato, ambaye aliwekwa kuwa gavana wa Yudea mwaka wa 26 W.K., alimruhusu Kayafa ashikilie cheo hicho katika kipindi cha miaka kumi ambacho Pilato alikuwa gavana. Kayafa alikuwa kuhani mkuu wakati wa huduma ya Yesu na hata kufikia mwanzoni mwa kazi ya kuhubiri ya wanafunzi wa Yesu. Lakini Kayafa alipinga ujumbe wa Kikristo.
Kumwogopa Yesu, Kuogopa Roma
Kayafa alimwona Yesu kuwa mtu hatari anayezusha fujo. Yesu alipinga jinsi viongozi Wayahudi walivyofasiri sheria za Sabato, naye akawafukuza wafanyabiashara na wale waliokuwa wakibadili pesa kutoka hekaluni, huku akisema kwamba wamelifanya hekalu kuwa “pango la wanyang’anyi.” (Luka 19:45, 46) Wanahistoria fulani wanasema kwamba masoko hayo ya hekalu yalikuwa mali ya familia ya Anasi, na huenda hiyo ni sababu nyingine iliyomfanya Kayafa ajaribu kumnyamazisha Yesu. Wakuu wa makuhani walipotuma maofisa ili wamkamate Yesu, walishangazwa na maneno yake hivi kwamba wakarudi mikono mitupu.—Yohana 2:13-17; 5:1-16; 7:14-49.
Kumbuka kilichotukia wakati viongozi wa kidini wa Wayahudi waliposikia kwamba Yesu amemfufua Lazaro. Injili ya Yohana inasema hivi: “Wakuu wa makuhani na Mafarisayo wakaikusanya pamoja Sanhedrini na kuanza kusema: ‘Tufanye nini, kwa sababu mtu huyu anafanya ishara nyingi? Tukimwacha hivyo, hao wote Yohana 11:47, 48) Washiriki wa Sanhedrini walimwona Yesu kuwa tisho kwa mamlaka ya kidini na kwa utaratibu katika jamii, na Pilato alikuwa amewakabidhi kazi hiyo. Ikiwa Waroma wangeona harakati zozote zile kuwa zingesababisha uchochezi, basi wangeingilia shughuli za Wayahudi, na Sanhedrini haikutaka hilo litukie kamwe.
watamwamini, na Waroma watakuja na kuondolea mbali mahali petu na taifa letu pia.’” (Ingawa Kayafa hangeweza kupinga kwamba Yesu alifanya kazi za ajabu, yeye hakumwamini Yesu bali alijitahidi kudumisha cheo chake na mamlaka yake. Je, kweli angeweza kukubali kwamba Lazaro alifufuliwa? Kwa kuwa Kayafa alikuwa Sadukayo, hakuamini ufufuo!—Matendo 23:8.
Uovu wa Kayafa ulifunuliwa wakati alipowaambia watawala wenzake hivi: “Hamwoni kwamba ni kwa faida yenu mtu mmoja afe kwa ajili ya watu kuliko taifa lote liangamizwe.” Simulizi hilo linaendelea kusema hivi: “Ingawa hivyo, hilo hakulisema kwa kujitungia mwenyewe; lakini kwa sababu alikuwa kuhani mkuu mwaka huo, alitoa unabii kwamba Yesu alikusudiwa kufa kwa ajili ya taifa, na si kwa ajili ya taifa hilo tu, bali ili watoto wa Mungu waliotawanyika huku na huku yeye apate pia kuwakusanya pamoja kuwa mmoja. Kwa hiyo tangu siku hiyo na kuendelea wakakata shauri kumuua [Yesu].”—Yohana 11:49-53.
Kayafa hakujua maana kamili ya maneno yake. Kwa kuwa alikuwa kuhani mkuu, alitoa unabii. * Si Wayahudi tu ambao wangefaidika na kifo cha Yesu. Dhabihu yake ya fidia ingewawezesha wanadamu wote kukombolewa kutoka katika utekwa wa dhambi na kifo.
Njama ya Mauaji
Wakuu wa makuhani na wazee Wayahudi walikusanyika nyumbani kwa Kayafa kuzungumzia jinsi watakavyomkamata na kumuua Yesu. Huenda kuhani mkuu alihusika katika kushauriana na Yudasi Iskariote kuhusu malipo ya kumsaliti Yesu. (Mathayo 26:3, 4, 14, 15) Hata hivyo, kumuua mtu mmoja tu hakungemwezesha Kayafa kufanikiwa katika maovu yake. ‘Sasa wakuu wa makuhani wakakata shauri kumuua Lazaro pia, kwa kuwa wengi kati ya Wayahudi walikuwa wakimwamini Yesu kwa sababu yake.’—Yohana 12:10, 11.
Malko, mtumwa wa Kayafa, alikuwa kati ya umati uliotumwa kumkamata Yesu. Kwanza, Yesu alipelekwa kwa Anasi ili kuhojiwa kisha akapelekwa kwa Kayafa, ambaye tayari alikuwa amewakusanya wazee Wayahudi ili wafanye kesi haramu ya hukumu usiku.—Mathayo 26:57; Yohana 18:10, 13, 19-24.
Kayafa aliendelea kutekeleza njama yake hata wakati mashahidi wa uwongo walipotoa ushuhuda unaopingana kumhusu Yesu. Kuhani mkuu huyo alijua maoni ya wapangaji njama wenzake kuhusu mtu yeyote aliyejifanya kuwa Masihi. Kwa hiyo, aliuliza ikiwa Yesu anadai kuwa Masihi. Yesu alijibu kwa kusema kwamba washtaki wake watamwona “akiwa ameketi kwenye mkono wa kuume wa nguvu na akija juu ya mawingu ya mbinguni.” Ili kujionyesha kuwa amejitoa kwa Mungu, ‘kuhani mkuu aliyararua mavazi yake ya nje, akisema: “Amekufuru! Tunahitaji mashahidi wengine wa nini?”’ Sanhedrini ikaamua kwamba Yesu anastahili kufa.—Mathayo 26:64-66.
Waroma ndio walioidhinisha adhabu ya kifo. Kwa kuwa Kayafa alikuwa mpatanishi kati ya Waroma na Wayahudi, huenda yeye ndiye aliyefikisha kesi hiyo kwa Pilato. Wakati Pilato alipotaka kumweka Yesu huru, huenda Kayafa alikuwa miongoni mwa wakuu wa makuhani waliopaaza sauti na kusema: “Mtundike mtini! Mtundike mtini!” (Yohana 19:4-6) Huenda Kayafa aliuhimiza umati kupiga kelele ili muuaji aaachiliwe badala ya Yesu, na huenda alikuwa miongoni mwa wakuu wa makuhani waliosema hivi kwa unafiki: “Sisi hatuna mfalme ila Kaisari.”—Yohana 19:15; Marko 15:7-11.
Kayafa alikataa uthibitisho ulioonyesha kwamba Yesu alifufuliwa. Aliwapinga Petro na Yohana, na akampinga Stefano pia. Isitoshe, Kayafa Mathayo 28:11-13; Matendo 4:1-17; 6:8–7:60; 9:1, 2) Hata hivyo, yapata mwaka wa 36 W.K., Vitelio, gavana Mroma wa Siria, alimwondoa Kayafa mamlakani.
alimwamuru Sauli kuwakamata Wakristo wote ambao angepata Damasko. (Maandishi ya Kiyahudi yanasimulia mambo mabaya kuhusu familia ya Kayafa. Kwa mfano, Talmud ya Babiloni inasema hivi: “Ole wangu kwa sababu ya nyumba ya Hanin [Anasi], ole wangu kwa sababu ya malalamiko yao,” au “fitina.” Inadhaniwa kwamba maneno hayo yanarejelea “mikutano ya siri ya kupanga njama za uonevu.”
Mambo Tunayojifunza Kutokana na Kayafa
Msomi mmoja anasema kwamba makuhani wakuu walikuwa watu “wagumu, wenye busara na wenye ustadi, na yaelekea walikuwa wenye majivuno.” Majivuno yalimfanya Kayafa asimkubali Masihi. Basi, hatupaswi kushangaa watu wanapokataa ujumbe wa Biblia leo. Wengine hawapendezwi sana na ukweli wa Biblia na hawataki kuacha imani wanazozipenda sana. Wengine wanaweza kufikiri kwamba kuwa wahubiri wanyenyekevu wa habari njema ni kujishushia heshima. Pia, watu wasio waaminifu na wenye pupa huchukia kanuni za Kikristo.
Akiwa kuhani mkuu, Kayafa angeweza kuwasaidia Wayahudi wenzake wamkubali Masihi, lakini tamaa yake ya kupata mamlaka ilimfanya amhukumu Yesu. Huenda aliendelea na upinzani huo hadi alipokufa. Masimulizi kuhusu mwenendo wake yanaonyesha kwamba si mifupa tu inayobaki mtu anapokufa. Kupitia matendo yetu, sisi hujifanyia jina la kudumu mbele za Mungu, yaani, jina bovu au jina zuri.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 9 Ili upate historia ya Wahasmoni, ona Mnara wa Mlinzi wa Juni 15, 2001, ukurasa wa 27-30.
^ fu. 19 Zamani, Yehova alimtumia Balaamu mwovu kutoa unabii mbalimbali wa kweli kuhusu Waisraeli.—Hesabu 23:1–24:24.
[Picha katika ukurasa wa 10]
Yosefu mwana wa Kayafa
[Picha katika ukurasa wa 10]
Sanduku la mifupa lililovumbuliwa hivi karibuni
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 10]
Ossuary, inscription, and cave in background: Courtesy of Israel Antiquities Authority