Anemia—Visababishi, Dalili, na Tiba
Beth anasema hivi: “Nilikuwa na tatizo la anemia nilipokuwa kijana. Nilichoka haraka sana, mifupa yangu iliuma, na nilipata shida kukaza fikira. Daktari aliniandikia dawa za kuongeza madini ya chuma. Nilitumia dawa hizo, na pia nikaboresha lishe yangu. Baada ya muda, nikaanza kupata nafuu.”
Tatizo la afya la Beth ni la kawaida. Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), watu bilioni mbili hivi, yaani, kama asilimia 30 ya watu ulimwenguni—wana tatizo la anemia. Katika nchi zinazoendelea, inakadiriwa kwamba asilimia 50 ya wanawake wajawazito na asilimia 40 ya watoto ambao hawajafikia umri wa kwenda shule wana tatizo hilo.
Anemia inaweza kuwa na madhara makubwa. Hali ikiwa mbaya sana, inaweza kufanya mtu awe na matatizo ya moyo. WHO inasema kwamba katika nchi fulani, anemia “inachangia asilimia 20% ya vifo vya akina mama.” Watoto wanaozaliwa na mama walio na upungufu wa madini ya chuma—aina ya kawaida zaidi ya anemia—wanaweza kuzaliwa kabla ya muda wao na wakawa na uzito mdogo. Watoto wenye anemia kawaida wanakua polepole na wanaweza kuambukizwa magonjwa kwa urahisi kuliko wengine. Lakini anemia inayotokana na upungufu wa madini ya chuma inaweza kuzuiwa au hata kutibiwa. a
Anemia Ni Nini?
Kwa maneno machache, watu wenye anemia hawana chembe nyekundu za kutosha zilizo na afya. Tatizo hilo linasababishwa na mambo mbalimbali. Wanasayansi wamegundua aina zaidi ya 400 za anemia! Linaweza kuwa tatizo la muda, tatizo la kuendelea, tatizo dogo au kubwa sana.
Ni Nini Kinachosababisha Anemia?
Anemia inasababishwa hasa na mambo matatu:
Kupungua kwa damu kunapunguza idadi ya chembe nyekundu mwilini.
Mwili hautokezi chembe nyekundu za kutosha zilizo na afya.
Mwili unaharibu chembe nyekundu.
Kupungua kwa madini ya chuma ndiyo aina ya anemia iliyoenea zaidi duniani. Mwili unapokosa madini ya chuma, hauwezi kutokeza hemoglobini ya kutosha, hemoglobini ni kitu kilicho ndani ya chembe nyekundu kinachowezesha chembe hizo kubeba oksijeni.
Ni Dalili Zipi Zinazoonyesha Mtu Ana Ukosefu wa Madini ya Chuma?
Mwanzoni, huenda tatizo la anemia likawa dogo, hata huenda lisigunduliwe. Ingawa kuna dalili mbalimbali, dalili za upungufu wa madini ya chuma mwilini zinatia ndani mambo yafuatayo:
Kuchoka kupita kiasi
Mikono na miguu baridi
Udhaifu
Kupauka kwa ngozi
Kichwa kuuma na kuhisi kizunguzungu
Maumivu ya kifua, mapigo ya moyo kwenda kasi, kushindwa kupumua
Kucha zinazovunjika kwa urahisi
Kukosa hamu ya kula, hasa kwa watoto
Tamaa ya kula barafu, wanga, au hata udongo
Ni Nani Wanaokabili Hatari ya Kuathiriwa?
Wanawake wanapatwa na upungufu wa madini ya chuma mara nyingi kwa sababu wanapoteza damu wakati wa hedhi. Wanawake wajawazito pia wako hatarini ikiwa hawali kiasi cha kutosha cha aina fulani ya vitamini B inayoitwa folate au folic acid.
Watoto wachanga wanaozaliwa kabla ya wakati au wale wenye uzito mdogo ambao hawapati madini ya chuma ya kutosha kutoka kwa maziwa ya mama au maziwa ya kopo.
Watoto ambao hawali vyakula mbalimbali vyenye afya.
Watu wasiokula nyama ambao hawali vyakula vya kutosha vyenye madini ya chuma.
Watu wagonjwa sana, kama walio na magonjwa ya damu, kansa, figo kuacha kufanya kazi, vidonda vya ndani vinavyovuja, au magonjwa mengine.
Jinsi ya Kutibu Anemia
Si aina zote za anemia zinazoweza kuzuiwa au kutibiwa. Lakini matatizo yanayotokana na ukosefu wa madini ya chuma au vitamini yanaweza kuzuiwa au kutibiwa kwa kula chakula kilicho na lishe bora inayotia ndani virutubisho vifuatavyo:
Madini ya chuma. Yanapatikana katika nyama, maharagwe, pojo, na mboga za majani ya kijani kibichi. b Pia kutumia vifaa vya kupika vyenye madini ya chuma kunaweza kuongeza madini hayo katika chakula.
Vitamini aina ya folate. Inapatikana katika matunda, mboga za majani ya kijani kibichi, njegere, maharagwe mekundu, jibini, mayai, samaki, lozi, na njugu karanga. Pia inapatikana katika vyakula vilivyoongezwa vitamini kama mikate, nafaka zinazopikwa viwandani, pasta, na mchele. Aina ya vitamini hiyo iliyotayarishwa kiwandani inaitwa folic acid.
Vitamini B-12. Inapatikana katika nyama, bidhaa zilizotengenezwa kwa maziwa, baadhi ya nafaka zinazopikwa viwandani, na bidhaa zilizotengenezwa kwa soya.
Vitamini C. Inapatikana katika matunda ya jamii ya chungwa na maji yake, pilipili, broccoli, nyanya, tikiti-maji, na stroberi. Vyakula vyenye vitamini C vinasaidia mwili wako kufyonza madini ya chuma.
Kila eneo lina vyakula vyake. Hivyo, chunguza ni vyakula vipi katika eneo lenu vilivyo na virutubisho muhimu. Hilo ni muhimu ikiwa wewe ni mwanamke, hasa ikiwa una uja-uzito, au unapanga kupata mtoto. Unapotunza afya yako, unapunguza uwezekano wa mtoto wako kupata ugonjwa wa anemia. c
a Habari katika makala hii kuhusu lishe na mambo yanayohusiana na hayo yametoka kwa Kliniki ya Mayo na kitabu The Gale Encyclopedia of Nursing and Allied Health. Ikiwa unafikiri kwamba una anemia, mwone daktari.
b Usitumie dawa za kuongeza madini ya chuma wala usimpe mtoto wako kabla ya kuzungumza na daktari. Madini hayo yakipita kiwango yanaweza kuharibu ini na kusababisha matatizo mengine.
c Pindi fulani madaktari wanamtia mgonjwa damu ili kutibu ugonjwa wa anemia, Mashahidi wa Yehova hawakubali matibabu hayo.—Matendo 15:28, 29.