Mihuri ya Kale Ilikuwa Nini?
Mihuri ya kale ilikuwa ni vifaa vidogo vilivyochongwa ishara fulani, ambayo kwa kawaida ilitumiwa kwenye udongo wa mfinyanzi au nta. Mihuri hiyo ilikuwa na maumbo mbalimbali, kama vile pia, mraba, micheduara, na hata maumbo ya kichwa cha mnyama. Mihuri ilitumiwa kuonyesha umiliki au kuthibitisha uhalali wa hati, na zilitumika kufunga mizigo au sehemu zilizo wazi, kama milango au mwingilio wa makaburi ya kale.
Mihuri iliundwa kwa vifaa mbalimbali kama mifupa, mawe ya chokaa, chuma, mawe ya thamani ya kadiri, au mbao. Wakati fulani majina ya mmiliki na ya baba yaliandikiwa kwenye mhuri. Mihuri fulani ilionyesha cheo cha mmiliki.
Ili kuthibitisha uhalali wa hati, mmiliki wa mhuri huo hukandamiza mchongo wake kwenye udongo wa mfinyanzi au nta au kitu kingine laini kwenye hati hizo. (Ayubu 38:14) Kitu hicho kingeganda na hivyo kuzuia watu wenye nia mbaya kuzipotosha hati hizo.
Mihuri Ilitumiwa Kuwakabidhi Wengine Majukumu
Mtu mwingine anaweza kupewa mhuri, na hivyo kupata mamlaka ya mmiliki wa mhuri huo. Mfano mmoja ni wa Farao wa Misri ya kale na mwanamume Mwebrania Yosefu, mwana wa mzee wa ukoo, Yakobo. Yosefu alikuwa mtumwa nchini Misri. Baadaye, alifungwa gerezani isivyo haki. Lakini mwishowe, Farao alimwachilia huru na kumpa cheo cha waziri mkuu. Biblia inasema: “Halafu Farao akaivua pete yake ya muhuri kutoka kwenye mkono wake mwenyewe na kumvisha Yosefu mkononi.” (Mwanzo 41:42) Kwa kuwa hiyo pete ya muhuri ilikuwa na mhuri rasmi, Yosefu alipata mamlaka ya kutekeleza kazi muhimu aliyopewa.
Malkia Yezebeli wa Israeli la kale alitumia muhuri wa mume wake alipopanga njama ya kumuua mwanamume aliyeitwa Nabothi. Kwa jina la Mfalme Ahabu, aliandika barua kwa wazee fulani, akiwataka wamsingizie Nabothi ya kuwa amemtukana Mungu. Kisha akaweka muhuri wa mfalme kwenye barua hizo na njama yake ya uovu ikafanikiwa.—1 Wafalme 21:5-14.
Mfalme Ahasuero wa Milki ya Uajemi alitumia pete ya muhuri ili kuthibitisha amri yake rasmi.—Esta 3:10, 12.
Mwandikaji wa Biblia Nehemia alisema kwamba wakuu wa Israeli, Walawi, na makuhani walionyesha wamekubali agano lililoandikwa kwa kutumia mihuri.—Nehemia 1:1; 9:38.
Biblia inataja pindi mbili ambazo mihuri ilitumika kulinda miingilio. Wakati fulani nabii Danieli alitupwa kwenye shimo la simba, “jiwe likaletwa na kuwekwa kwenye mwingilio wa shimo hilo.” Basi, Mfalme Dario, mtawala wa Umedi na Uajemi, “akalitia muhuri kwa pete yake ya muhuri na kwa pete ya muhuri ya wakuu wake ili uamuzi kumhusu Danieli usibadilishwe hata kidogo.”—Danieli 6:17.
Mwili wa Yesu Kristo ulipowekwa ndani ya kaburi, maadui wake “wakaenda na kulilinda kaburi kwa kulitia jiwe muhuri,” jiwe ambalo lilivingirishwa mpaka kwenye mwingilio. (Mathayo 27:66) Kitabu kimoja kinachofafanua Biblia kilichoandikwa na Matthew by David L. Turner kinasema kwamba ikiwa ulikuwa muhuri rasmi uliowekwa na mamlaka ya mfalme, basi “huenda muhuri uliowekwa ulikuwa wa udongo wa mfinyanzi au nta uliochomekwa kwenye upenyo wa . . jiwe lililo kwenye mwingilio wa kaburi.”
Kwa kuwa mihuri ya kale inaweza kutueleza mengi kuhusu mambo ya zamani, wachimbuaji wa vitu vya kale na wanahistoria huichunguza sana. Kwa kweli, somo la mihuri, linaloitwa sigillography, ni nyanja kubwa ya uchunguzi.