Lightbearer Yapeleka Nuru ya Kiroho Kusini Mashariki Mwa Bara la Asia
Mwazoni mwa miaka ya 1930, Indonesia, Malasia, na ile ambayo sasa inaitwa Papua New Guinea, hazikuwa zimehubiriwa kwa kiasi kikubwa na Mashahidi wa Yehova. Habari njema ingefika jinsi gani katika nchi hizi? Kutokana na uhitaji huo ofisi ya tawi ya Australia (ambayo sasa ni ya Australasia) ilinunua mashua inayotumia injini na iliyo na milingoti miwili yenye urefu wa mita 16. Ilipewa jina Lightbearer kwa sababu wote waliosafiri katika mashua hiyo walikuwa mapainia, a nao walitumia mashua hiyo kuangaza nuru ya kiroho katika nchi za mbali.—Mathayo 5:14-16.
Kuhubiri New Guinea
Februari 1935, wasafiri hao saba walitoka kaskazini mwa Sydney, iliyo pwani ya Australia, wakielekea Port Moresby huko New Guinea. Walivua samaki njiani na kusimama katika bandari kadhaa ili kuongeza mafuta, kununua chakula cha ziada, na kufanyia mashua marekebisho. Aprili 10, 1935 walianza tena safari yao kutoka Cooktown huko Queensland. Walitumia injini ya mashua walipokuwa wanapita sehemu hatari yenye tumbawe kubwa la Australia. Lakini injini ilianza kutoa sauti isiyo ya kawaida hivyo ilibidi waizime. Swali lilikuwa ni: Je, warudi au waendelee na safari mpaka New Guinea? Nahodha wa mashua, Eric Ewins alisema hivi “hatuwezi kuwazia hata kidogo kurudi.” Hivyo mashua ya Lightbearer iliendelea na safari na kufika Port Moresby salama Aprili 28, 1935.
Fundi alipokuwa akiendelea kurekebisha injini, kikundi hicho chote, isipokuwa Frank Dewar, kilienda kuhubiri habari njema jijini Port Moresby. Frank, aliyetajwa na mwanamume mmoja kama “painia mwenye nguvu na bidii” alisema hivi: ‘Nilibeba mzigo mkubwa wa vitabu na kutembea navyo kilomita kama 32 au zaidi kutoka ufukweni nikiwahubiria wakazi wa eneo hilo.’ Alipokuwa akirudi, alipita njia tofauti ambayo alihitaji kuvuka mto mdogo uliokuwa na mamba. Lakini alikuwa makini na akafanikiwa kurudi salama. Bidii ya wahubiri hao ilikuwa na matokeo mazuri. Baadhi ya watu waliokubali machapisho ya Biblia wakati huo baadaye walikuwa Mashahidi wa Yehova.
Kuhubiri Java
Baada ya kurekebisha injini, Lightbearer iliondoka Port Moresby na kuelekea kisiwa cha Java kilicho Dutch East Indies (ambayo sasa ni Indonesia ). Baada ya kusimama katika vituo kadhaa ili kupata mahitaji yao, hatimaye Julai 15,1935, kikundi hicho kilifika Batavia (ambayo sasa ni Jakarta).
Walipofika Jakarta, painia mmoja kati yao aliyeitwa Charles Harris alibaki na kuendelea kuhubiri habari njema kwa bidii. b “Alisema hivi: “Siku hizo, kazi yetu ya kuhubiri ilihusisha hasa kugawa machapisho ya Biblia na kisha kwenda mji unaofuata. Nilibeba machapisho katika Kiarabu, Kichina, Kiholanzi, Kiindonesia na Kiingereza. Watu walikubali machapisho yetu hivyo niligawa kama nakala 17,000 kwa mwaka.”
Bidii ya Charles ilionekana na wenye mamlaka. Wakati fulani, ofisa mmoja alimuuliza Shahidi mwingine aliyekuwa akihubiri Java, ni Mashahidi wangapi waliokuwa wakihubiri Java Mashariki, kule Charles alipokuwepo. Ndugu huyo alimjibu, “Mmoja tu.” Ofisa akasema kwa hasira, “Kweli unatarajia niamini hilo? Lazima mtakuwa na jeshi kubwa la wafanyakazi huko ukilinganisha na idadi ya machapisho yaliyosambazwa.”
Kuhubiri Singapore na Malasia
Lightbearer ilitoka Indonesia na kufika Singapore Agosti 7. Kila mara waliposimama, walicheza rekodi za hotuba wakitumia spika na kipaza sauti chenye nguvu kilicho kwenye mashua. Mara nyingi, njia hii ya kuhubiri habari njema ilipata wasikilizaji wengi. Hata wanahabari wa gazeti la Singapore Free Press walisema kwamba “usiku wa Jumatano sauti kubwa sana ilisikika kutoka majini . . . ikitoka katika . . . mashua inayoitwa ‘Light bearer’ iliyotoka Australia, nayo imekuwa ikitangaza programu za Mnara wa Mlinzi nchini Singapore.” Ripoti hiyo pia ilisema kwamba “hali zilipokuwa shwari programu hizo ziliweza kusikika umbali wa kilomita . . . tatu mpaka nne.”
Mashua ya Lightbearer ilipokuwa Singapore, Frank Dewar aliondoka ili kuanza mgawo mpya. Anakumbuka hivi: “Tulipoondoka, tulianza kuhubiri Singapore huku tukiishi ndani ya mashua. Muda ulipofika wa Lightbearer kuondoka, Eric Ewins alinishtua kwa kusema, ‘Frank ulisema umechagua Siam (ambayo sasa ni Thailand) kuwa eneo lako la kuhubiri. Tutakuacha hapa. Haya, nenda sasa! Nilishangaa na kusema: ‘Lakini hata sijui Siam ni wapi kutoka hapa!’” Eric akamwambia Frank kwamba anaweza kufika Siam kwa kutumia treni inayotoka Kuala Lumpur, ambayo sasa ni Malasia. Frank alitii na kuelekea Kuala Lumpur ili kupanda treni kisha akafika Thailand miezi kadhaa baadaye. c
Lightbearer ilipokuwa inasafiri kuelekea pwani ya magharibi mwa Malasia, ilipita Johore Bahru, Muar, Malacca, Klang, Port Swettenham (ambayo sasa ni Port Klang), na Penang. Na katika kila bandari, kikundi hicho kilicheza rekodi za hotuba zilizotegemea Biblia kwa kutumia spika za mashua hiyo. Jean Deschamp, Shahidi aliyekuwa akitumikia nchini Indonesia alisema kwamba “hata ndege kubwa yenye umbo la sahani isingewavutia watu kwa kiasi kikubwa hivyo.” Baada ya kucheza rekodi hizo, kikundi chote kilienda ufukweni na kuwapatia watu waliopendezwa machapisho.
Kuhubiri Sumatra
Kutoka Penang, kikundi chote kilisafiri kupitia Mlango Bahari wa Malacca kuelekea Medan, Sumatra (ambayo sasa ni sehemu ya Indonesia). Eric Ewins anakumbuka na kusema, “Tulifurahia na kusisimka sana tulipokuwa katika wilaya ya Medan, watu wengi walisikiliza habari njema.” Akina ndugu waligawa nakala 3,000 hivi huko.
Lightbearer iliendelea kuelekea kusini na kikundi hicho kiliendelea kuhubiri katika bandari kubwa zilizopo upande wa mashariki mwa Sumatra. Novemba 1936, mashua ilirudi Singapore na Eric Ewins akaondoka. Majuma machache baadaye alimwoa Irene Struys, Shahidi aliyekuwa anaishi Singapore. Wakiwa pamoja Eric na Irene waliendelea na upainia huko Sumatra. Bila shaka, sasa Lightbearer ilihitaji kapteni mpya.
Kuhubiri Borneo
Kapteni mpya alikuwa Norman Senior, baharia mwenye ujuzi. Alifika kutoka Sydney Januari 1937. Kisha kikundi hicho kikasafiri kutoka Singapore kuelekea Borneo na Celebs (ambayo sasa ni Sulawesi), ambapo walihubiri kufikia umbali wa kilomita 480 kwenye nchi kavu.
Lightbearer ilipofika bandari ya Samarinda, iliyo kwenye kisiwa cha Borneo, msimamizi wa bandari hakuwaruhusu wawahubirie watu katika eneo hilo. Hata hivyo, Norman alimweleza jinsi kazi yetu ya kuhubiri inavyofanywa, naye akatuelewa na hata akachukua machapisho kadhaa.
Katika pindi nyingine, kiongozi wa kanisa fulani alimwalika Norman ahubiri katika kanisa lake. Lakini badala ya kutoa hotuba yeye mwenyewe, Norman alicheza rekodi tano za Biblia kwa kutumia gramafoni, na kiongozi huyo aliitikia vizuri. Hata alichukua machapisho kadhaa kwa ajili ya rafiki zake. Hata hivyo, itikio la kiongozi huyo wa dini lilikuwa tofauti. Kwa ujumla, makasisi wa dini hawakufurahishwa na kazi ya Mashahidi wa Yehova. Ukweli ni kwamba walichukizwa na ujasiri wa kikundi hicho na hata kuchochea wenye mamlaka wazuie mashua ya Lightbearer isiingie kwenye baadhi ya bandari.
Kurudi Australia
Kwa sababu ya marufuku iliyochochewa na makasisi, Desemba 1937 Lightbearer ilirudi Australia. Kikundi hicho kilitia nanga bandari ya Sydney wakati barabara wa kuhudhuria kusanyiko la Mashahidi wa Yehova lililofanyika Aprili 1938. Hiyo ilikuwa zaidi ya miaka mitatu tangu Lightbearer ilipoondoka Sydney. Mashua hiyo iliuzwa mwanzoni mwa miaka ya 1940, baada tu ya kazi ya Mashahidi kupigwa marufuku nchini Australia. Ndugu Ewins alisema, “Bila shaka mashua hiyo ilitimiza kusudi lake.” Pia, alifafanua muda wake wa utumishi akiwa na Lightbearer kwa kusema, “Ilikuwa miaka yenye furaha zaidi maishani mwangu.”
Kumbukumbu ya Kudumu ya Lightbearer
Kikundi cha wasafiri wa Lightbearer walipanda mbegu za Ufalme katika eneo kubwa lenye watu wengi. Na licha ya upinzani, hatua kwa hatua kazi yao ilizaa matunda. (Luka 8:11, 15) Kwa kweli, katika nchi zote ambazo mapainia hao walihubiri, sasa kuna wahubiri wa Ufalme zaidi ya 40,000. Hiyo ni kumbukumbu nzuri kama nini iliyoachwa na wanaume wachache wenye ujasiri pamoja na mashua yao iliyoitwa kwa jina lililopatana na kusudi lake!