SOMO LA 23
Jinsi Machapisho Yetu Yanavyoandikwa na Kutafsiriwa
Ili tufanikiwe kutangaza “habari njema” katika “kila taifa na kabila na lugha na watu,” tunachapisha vitabu na magazeti katika lugha zaidi ya 750. (Ufunuo 14:6) Kazi hiyo yote inafanywaje? Tuna waandishi katika nchi mbalimbali na vilevile vikundi vya watafsiri. Wote hao ni Mashahidi wa Yehova.
Makala ya kwanza huandikwa katika Kiingereza. Baraza Linaloongoza husimamia kazi ya Halmashauri ya Uandikaji katika makao yetu makuu. Halmashauri hii huratibu kazi za waandikaji wanaoishi katika makao makuu na pia wale walio katika baadhi ya ofisi za tawi. Kwa sababu Halmashauri ya Uandikaji inatumia waandikaji wa nchi mbalimbali, machapisho yetu huwapendeza watu wa mataifa yote.
Makala hutumwa kwa watafsiri. Baada ya kuandikwa na kuidhinishwa, makala hutumwa kwa vikundi vya watafsiri duniani kote. Watafsiri hao hujitahidi kuchagua “maneno sahihi ya kweli” yanayotafsiri maana kamili katika lugha yao.—Mhubiri 12:10.
Kompyuta huharakisha kazi. Kompyuta haiwezi kufanya kazi zinazofanywa na waandikaji na watafsiri. Hata hivyo, kazi hiyo inaweza kuharakishwa kwa kutumia kamusi zilizo kwenye kompyuta, pamoja na vifaa vingine vya kufanyia utafiti. Mashahidi wa Yehova walibuni programu ya kompyuta inayoitwa Multilanguage Electronic Publishing System (MEPS). Programu hiyo huwezesha maandishi yaliyotafsiriwa katika mamia ya lugha kuunganishwa pamoja na picha, na kuyatayarisha kwa ajili ya uchapishaji.
Kwa nini tunafanya kazi yote hiyo ya uchapishaji, hata katika lugha zinazozungumzwa na watu wachache tu? Kwa sababu ni mapenzi ya Mungu kwamba “watu wa namna zote waokolewe na kupata ujuzi sahihi wa kweli.”—1 Timotheo 2:3, 4.
-
Machapisho yetu huandikwa jinsi gani?
-
Kwa nini tunatafsiri machapisho yetu katika lugha nyingi sana?